Dili zikitiki Tanzania Prisons kazi mnayo!

VIONGOZI wa timu ya Tanzania Prisons wanaendelea na vikao vya tathmini mkoani Dodoma, ili kupata picha ya kipi wakifanye katika usajili wa dirisha dogo litakalofungwa Januari 30, lakini kama michongo yao itatiki wapinzani waliopo katika Ligi Kuu Bara itabidi wajipange mapema.

Prisons imecheza mechi saba imeshinda mbili, imetoka sare moja na imefungwa nne, imekusanya pointi saba na ipo nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu inayorejea Januari 21, hivyo baada ya tathimini watajua kipi wakiboreshe katika kikosi.

Kabla ya kikao hicho Mwanaspoti liliandika wachezaji ambao walishaanza kuzungumza nao ambao ni Gadiel Michael, Ayubu Lyanga, Kelvin Kijili kutoka Singida Black Stars na Tepsi Evance anayecheza KMC kwa mkopo kutoka Azam FC.

“Kuhusu Gadiel, Lyanga na Kijili kilichokwamisha ni SBS kufungiwa kusajili na Evance bado mazungumzo yanaendelea, lakini kikao kinachofanyika Dodoma ndicho kitakachotoa picha kamili ya nani ataondolewa na nani ataendelea kusalia,” kilisema chanzo hicho.

Mbali na hilo chanzo hicho kilisema pamoja na viongozi kuendelea na vikao, timu ilishaingia kambini tangu Jumapili na inaendelea na mazoezi kama kawaida.

“Tunatarajia kucheza mechi ya kirafiki na Mbeya City Januari 11 Jumapili kama mambo yatakwenda sawa, itachezwa Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa meneja wa timu hiyo, Benjamin Asukile amesema: “Timu inaendelea na mazoezi, kuhusu hayo mengine watafute viongozi ndiyo wenye nafasi ya kuyazungumzia.”