Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Asha-Rose Migiro amewataka viongozi waliopewa dhamana za kuongoza kitaifa kupitia chama hicho, kuhakikisha wanashiriki kila kikao cha CCM ngazi ya mashina yao kujua yanayoelezwa na wananchi.
Viongozi waliotajwa na Dk Migiro, ni wa chama hicho ngazi za Taifa na wale wa Serikali ambao ama dhamana zao zimetokana na CCM au wenyewe pia ni wanachama wa chama hicho.
Maelekezo hayo ya mtendaji mkuu huyo wa CCM, yanalenga kudumisha imani ya wananchi kwa chama hicho, kwa kuhakikisha njia za kusikiliza na kujua changamoto zao zinaongezeka na zishughulikiwe.
Dk Migiro ametoa maelekezo hayo leo, Ijumaa Januari 9, 2025 alipowahutubia wananchi wa Ubungo na Kinondoni, jijini Dar es Salaam, katika mwendelezo wa ziara yake kwa wananchi wa jiji hilo.
Amesema kila mwanachama wa CCM wakiwemo viongozi wa chama hicho na Serikali kitaifa, kuhakikisha anashiriki vikao vya ngazi ya mashina kusikiliza kero za wananchi na kuona namna ya kuzitatua.
“Nitaomba ndugu zangu mabalozi muwe huru. Tujue mwenendo wa vikao vyetu kwenye mashina ili kwenye changamoto tushirikiane,” amesema.
Amesema hata kama ni kiongozi wa CCM amepata dhamana ya kuwawakilisha wananchi ngazi ya kitaifa, wahakikishe wanashiriki na kwamba wasisubiri kuitwa na wajumbe.
Ameeleza vikao hivyo vinafanyika kila mwezi hivyo wasiwaachie wajumbe wa mashina na wanachama ambao wanaishia kulalamikiana bila kupata utatuzi.
Kwa kuwa uhai wa CCM unatokana na mashina, amesema vikao hivyo vitawezesha kujipima kwa kiwango gani chama hicho kinakubalika na kupendwa na wananchi.
Amewataka washiriki kikamilifu kwenye vikao hivyo, ili kupata taarifa za yanayoendelea, kubadilishana uzoefu wa yanayoendelea katika chama na jamii.
“Rai yangu kwenu viongozi wote tufanye shughuli zetu kwa uwazi na uwajibikaji ili wanachama wake kitu gani kipo kwenye chama chatu ili waijue nini wanakuja kutushauri ili kutuletea kwa maslahi ya chama chetu,” amesema.
Kwa kuwa wanaishi na watu, amewataka wajenge utu na wasijitenge na jamii kwani uhalali wa chama hicho unatokana na uhusiano wake wa karibu na wananchi.
Amesema viongozi na wanachama wana dhima ya kutafsiri kaulimbiu ya Kazi na Utu, Tunasonga Mbele kwa kuhakikisha wanajenga mahusiano mema na jamii.
“Tuonekane tushirikiane na tushikamane kila pale inapotokea changamoto katika jamii. Kuna matatizo yanayochukua muda tunao madiwani na wabunge wawe daraja la kufahamu kero zetu na kuleta mrejesho kwa wananchi,” amesema.
Pamoja na hayo, ametaka ngazi za mashina ziandaliwe utaratibu wa mafunzo kwa wanachama ili waielewe historia ya chama hicho na hatimaye kuzalisha viongozi bora.
Pia, ametaka ameahidi kukaa na kuangalia upya ukubwa wa mashina ili yapunguzwe na kuwawezesha mabalozi kuyasimamia kwa weledi.
Awali, akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo amesema tayari Serikali imeshatafsiri maudhui ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2025/30) na kuyapelekea kuwa mpango wa kwanza wa maendeleo wa mwaka 2025/26 hadi 2030/31.
Amesema mapema wiki hii baraza la mawaziri katika kikao chake, limeshaupitisha mpango huo wa maendeleo na kwamba kinachosubiriwa ni kwenda kuuwasilisha bungeni tayari kwa utekelezaji.
Sambamba na hilo, ameeleza tayari wameshaanza utekelezaji wa Ilani ya CCM katika majimbo yote ya wilaya za Ubungo na Kinondoni kwa kufanya ziara kadhaa za wabunge na madiwani kwenye Kata na Mitaa.
Hata hivyo, amesema kipaumbele cha kwanza katika majimbo yote ni utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara, ambayo ndio kero kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambuke amesema viongozi wa Serikali wataendelea kusimamia kazi zinazofanywa na viongozi wa kitaifa.
“Tutaisimamia miradi hii kuhakikisha inakamilika kwa haraka, ubora na ufanisi ili adhma na dhamira ya Serikali ya kutaka huduma bora za usafiri inatimizwa,” amesema Albert Ngata Balozi wa Shina Namba 1.
Amesisitiza kila shilingi inayotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo inatumika inavyopaswa bila ubadhirifu.
Ameomba mabalozi hao kupatiwa vitambulisho ili watambulike wanapotekeleza majukumu yao, hata katika Serikali za Mitaa.
Sambamba na hilo, ameomba kupunguziwa idadi ya nyumba wanazozisimamia, ili kumudu usimamizi na utambuzi wa yeyote anayeingia na kutoka katika maeneo wanayoongoza.
Pia, ameomba angalau wanapostaafu kuwepo na utaratibu wa kupatiwa zawadi ya kutambua mchango wa utendaji wao, ili iwe kumbukumbu ya utumishi wao ngazi ya Serikali za Mitaa.
