Kiungo Simba atua Mbeya City

KIUNGO wa Simba aliyekuwa anacheza kwa mkopo Mashujaa, Omary Omary amekamilisha usajili wa mkopo wa miezi sita kuitumikia Mbeya City.

Omary ambaye alijiunga na Simba akitokea Mashujaa na baadaye kurudishwa kwa mkopo ameliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli amemalizana na City kwa mkopo wa miezi sita anaamini huko atapata wakati mzuri wa kucheza.

“Ni kweli namalizia msimu na City baada ya makubaliano ya kusaini mkataba wa mkopo wa miezi sita, naamini huko itakuwa sehemu sahihi kwangu kurudi kwenye ushindani kama nitapata nafasi ya kucheza mara kwa mara,

“Kwa mujibu wa mkataba wangu ni kupata kipaumbele cha kucheza natamani kurudi sokoni dirisha kubwa, hivyo miezi sita nitakayoipata City itaamua kubaki au kusonga mbele zaidi.”

Akizungumzia msimu huu kwa ujumla, Omary amesema ni msimu mgumu na amejiunga na timu ambayo inajipambania kuhakikisha inaendelea kubaki Ligi Kuu baada ya kupanda msimu huu hivyo anaamini ni sehemu sahihi.

“Msimu huu ni wa ushindani ligi imechezwa mechi chache, lakini zimetoa picha ya ushindani mkubwa uliopo hivyo baada ya kumalizana na City mchakato uliopo ni kuhakikisha naipambania nembo ya timu hiyo ili iendelee kubaki Ligi Kuu.

“Kucheza timu kama Mbeya City ambayo imetoka kupanda ligi na inaongeza wachezaji wazoefu ili kuipambania ni sehemu ya sahihi kwangu mimi binafsi kuipambania timu na kujipambania mwenyewe ili niweze kuonyesha nilichonacho.”