Kula vyakula hivi unukie vizuri kiasili

Mwanza. Je, unajua chakula unachokula kinaweza kuamua jinsi mwili wako unavyonukia? Iwapo unashughulika na harufu mbaya ya mwili au pumzi isiyovutia, suluhisho linaweza kuwa ndani ya sahani yako ya chakula.

Sayansi inaonyesha kuwa vyakula fulani vinaweza kusaidia mwili kupunguza bakteria wanaosababisha harufu mbaya na kukufanya harufu nzuri au mtu anukie vizuri kwa njia ya asili.

Kula vyakula vya asili vyenye afya kunaweza kuboresha harufu ya mwili, pumzi na ngozi. Wataalamu wanasema lishe ni sehemu muhimu ya afya ya mwili, na kuchagua vyakula sahihi kunaweza kukufanya harufu nzuri bila kutegemea manukato au harufu za kutengeneza.

Harufu ya mwili hutokana zaidi na bakteria wanaobadilisha jasho mwilini. Jasho lenyewe halina harufu mbaya bali ni bakteria hufanya kazi hiyo, hivyo ulaji wa vyakula vyenye antioxidants, probiotics, na chlorophyll husaidia kupunguza bakteria hao na kudhibiti harufu mbaya.

Dk Pendo Mushi, daktari wa lishe katika Hospitali ya Kaloleni jijini Arusha, anasem: “Kuna vyakula vinavyosaidia mwili kunukia vizuri kiasili, kwa sababu huathiri harufu ya jasho, pumzi na hata ngozi. Vyakula hivi husaidia mwili kupunguza bakteria wanaosababisha harufu mbaya na kuboresha afya kwa ujumla.”

 Matunda yenye maji mengi, mboga za majani 

Dk Pendo anatolea mfano, ulaji wa matunda kama tikiti maji au nanasi si tu unakupa maji ya kutosha mwilini bali pia huondoa bakteria wanaosababisha harufu mbaya.

Pia, mboga za majani kama mchicha au spinachi kwenye mlo wa kila siku, kunasaidia usagaji chakula vizuri na kupunguza gesi tumboni, jambo linaloathiri harufu ya mwili.

Utafiti wa majaribio wa mwaka 2024 uliofanywa Ulaya na Marekani (Applied Sciences Randomized Controlled Trials) uliojumuisha washiriki 60 waliopewa vyakula vyenye kemikali za asili zinazopatikana kwenye matunda na mboga zinazosaidia kuondoa bakteria na sumu mwilini,  ulionesha ulaji wa vyakula hivyo ulipunguza harufu mbaya ya mwili kwa kuzuia baadhi ya visababishi vya harufu mbaya inayotokana na bakteria mwilini.

Kwa mujibu wa Dk Pendo, matunda yenye maji mengi kama vile  tikiti maji, nanasi, chungwa, embe ambayo yana antioxidants (visafisha sumu mwilini na kupunguza bakteria), husaidia mwili kusafisha mfumo wake na kupunguza harufu mbaya.

Anasema matunda ya jamii ya berries kama strawberry na blueberry yenye maji na nyuzi nyingi, husababisha mwili kuwa na harufu ya asili yenye kuvutia na kufurahisha.

“Mboga za majani mabichi yaani mfano spinachi, mchicha, lettuce zina chlorophyll (kiambata cha mimea kinachosafisha mwili kwa kupunguza harufu mbaya) na nyuzi zinazosaidia utumbo kufanya kazi vizuri,”anasema.

Anasema tangawizi ambayo inasifika kwa kusaidia mmeng’enyo wa chakula,  pia hupunguza harufu mbaya ya mwili kwa kuboresha usagaji chakula na kupunguza gesi tumboni.

Anaendelea kusema, mdalasini na iliki licha ya kutoa harufu nzuri kwenye vinywaji,   viungo hivyo vinatoa harufu nzuri ya asili na husaidia kupunguza bakteria wanaoweza kuchangia harufu mbaya.

Mtindi wa asili ni miongoni mwa lishe inayotajwa kupunguza harufu mbaya kwakuwa una bakteria wazuri wanaosaidia afya ya utumbo na  husaidia microbiome ya utumbo kuwa imara, kupunguza uzalishaji wa misombo yenye harufu mbaya.

Mimea tiba kama basil,  rosemary, mnanaa  na parsley zina uwezo wa kusaidia mwili kunukia vizuri kiasili kutokana na uwepo wa kemikali za asili zinazosaidia kuua bakteria.

Akizungumza na jarida la afya la Health, mtaalamu wa lishe na Meneja wa Afya katika Hospitali ya Providence St. Jude Medical Center ya nchini Marekani, Megan Wroe anasema mimea hiyo pia ina mafuta ya asili yenye harufu nzuri.

“Mimea hii inapotafunwa, mafuta yake ya asili hutoka na kutoa harufu nzuri, kiasi kwamba mtu anaweza kunukia kama aliyekula pipi za kusafisha pumzi,” anasema Wroe.

Akifafanua zaidi, Dk Heewon Gray, Mhadhiri wa lishe katika Chuo Kikuu cha South Florida nchini Marekani, anasema majani ya mnanaa yana misombo ya asili iitwayo polyphenols (kemikali za mimea zinazosaidia kupunguza harufu mbaya).

Kwa mujibu wa Dk Gray, aliyenukuliwa katika maelezo ya kitaalamu kuhusu lishe na afya ya kinywa, misombo hiyo hufanya kazi kwa kupunguza kemikali za salfa, ambazo ndizo chanzo kikuu cha harufu mbaya ya mdomo.

Kazi za kitafiti zimeonyesha kuwa kutafuna majani mabichi ya mnanaa au kutumia mafuta yake hupunguza idadi ya bakteria wanaosababisha harufu mbaya ya kinywa na magonjwa ya fizi, hali inayoboresha harufu ya pumzi kwa ujumla.

Mbali na mimea tiba, wataalamu wanasema karanga na vyakula vya mbegu, vina mchango mkubwa katika kuboresha harufu ya mwili.

Kwa mujibu wa Dk Gray, vyakula kama mbegu za maboga, korosho, mbegu za linzi (flaxseeds) na walnuts vina virutubisho muhimu ikiwemo zinc, omega-3 ya mimea, vitamini E, na polyphenols.

“Virutubisho hivi huathiri muundo wa mafuta ya ngozi, usawa wa bakteria wa ngozi na hali ya kemikali mwilini, mambo ambayo kwa njia isiyo ya moja kwa moja huamua harufu ya mwili,” anasema Gray.

Anasema uwiano mzuri wa mafuta mwilini na ngozi yenye afya husaidia kupunguza kuoza kwa mafuta ya ngozi na jasho, hali inayosababisha harufu mbaya kama ya uvundo.

Aidha, virutubisho hivyo husaidia kudumisha afya ya bakteria wazuri wa ngozi, na hivyo kupunguza uzalishaji wa misombo ya kemikali yenye harufu mbaya.

Ushahidi wa kisayansi unaunga mkono maelezo hayo. Utafiti uliofanywa mwaka 2018 nchini Japan na Dk Naoki Suzuki, Mhadhiri na mtafiti wa afya ya kinywa, ulibaini kuwa ioni za zinc zina uwezo mkubwa wa kupunguza harufu mbaya ya mdomo.

Utafiti huo, uliochapishwa katika jarida la Journal of Applied Oral Science, ulibaini kuwa zinc hufanya kazi kwa njia mbili, ikiwemo kudhibiti bakteria wanaosababisha harufu na kupunguza kemikali za salfa zinazohusika moja kwa moja na harufu mbaya ya mdomo.

Naye, Wroe anasema mbegu za bizari (fennel seeds) zina uwezo wa kipekee wa kuboresha harufu ya mwili kwa ujumla.

Anasema kutafuna mbegu hizo baada ya kula husaidia kusafisha kinywa, huku pia zikichochea uzalishaji wa mate mengi zaidi ambayo husafisha mdomo.

“Antioxidants zilizopo kwenye mbegu za bizari husafiri hadi kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na kusaidia kuondoa bakteria wanaosababisha gesi zenye harufu mbaya tumboni,” anasema.

Hata hivyo, wataalamu wanasema kula vyakula vinavyosaidia kunukia vizuri hakutoshi bila kuepuka vyakula vinavyochochea harufu mbaya.

Kwa mujibu wa Wroe, ulaji wa vyakula vilivyosindikwa kupita kiasi kama vile vyakula vya kukaanga sana, vitafunwa vya viwandani, vinywaji vyenye sukari nyingi na chakula chenye nyuzi chache husababisha mmeng’enyo wa chakula kuwa wa taratibu.

“Mmeng’enyo unapokuwa wa taratibu, chakula huchacha tumboni na kuzalisha gesi zenye harufu mbaya ambazo hujitokeza kupitia pumzi au jasho,” anasema Wroe.

Anasema mtindo mbaya wa maisha hufanya mwili ushindwe kuondoa sumu ipasavyo, hali inayosababisha jasho lenye harufu kali, hasa kwa watu wanaokula nyama yenye mafuta mengi na vyakula vya jamii ya vitunguu kama kitunguu saumu na vitunguu maji.

Utafiti uliofanywa katika chuo kikuu cha Charles kilichopo Jamhuri ya Czechia mwaka 2006 uliojumuisha wanaume 44 waliokula lishe tofauti kwa wiki mbili, baadhi wakila chakula kisicho na nyama nyekundu na wengine wakila chenye nyama hiyo, ulionesha wanaume waliokuwa kwenye lishe isiyo na nyama walionekana kuwa na harufu ya mwili nzuri na kuvutia zaidi, ikilinganishwa na wale waliokula nyama nyekundu.

Wroe anasisitiza kuwa njia bora ya kudhibiti harufu mbaya ya mwili ni kubadilisha mlo wa kila siku.

“Kinga ya harufu mbaya ni bora kuliko tiba. Hata hivyo, suluhisho za haraka kama kutafuna mnanaa, mbegu za bizari au kula matunda yenye maji mengi zinaweza kusaidia pale mtu anapopata harufu mbaya ya ghafla,” anasema.