MAAFISA POLISI KANDA YA ZIWA WANOLEWA, WAHIMIZWA KUTOJIFUNGIA OFISINI

::::::

Kamishna wa Polisi Jamii, CP Faustine Shilogile, amewataka Maafisa wa Polisi Jamii kuwajibika ipasavyo kwa kutoka maofisini na kuwahudumia wananchi moja kwa moja katika jamii.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku moja yaliyofanyika katika ukumbi wa Rock City Mall wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza kwa Maafisa wa Polisi Jamii wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kamishna Shilogile alisema kuwa dhana ya Polisi Jamii ni nyenzo muhimu katika kujenga mahusiano ya karibu kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, jambo ambalo husaidia kubaini mapema viashiria vya uhalifu na kuvizuia kabla havijatokea.

Mafunzo hayo yameshirikisha Maafisa kutoka mikoa sita ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mara, Tarime-Rorya, Simiyu, Geita, Tabora na Shinyanga. Mada zilizotolewa ni pamoja na: Dhana ya Polisi Jamii, Mawasiliano wakati wa migogoro, Kupinga ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto na Utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, CP Shilogile amewahimiza Maafisa hao kuhakikisha kuwa maarifa na ujuzi walioupata kupitia mafunzo haya yanawafikia Askari walioko chini yao ili kuimarisha utekelezaji wa dhana ya Polisi Jamii kwa vitendo katika ngazi ya jamii.

Pia amewakumbusha kuanzisha na kubuni miradi bunifu ya Polisi Jamii itakayochangia katika kupunguza uhalifu na kuimarisha usalama wa wananchi katika maeneo yao.