OFISA Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Mohamed Kabwanga, amesema kilichotokea katika maandalizi ya Kombe la Mapinduzi 2026, kimewapa chachu ya kuboresha Ligi Kuu Zanzibar.
Kabwanga amesema kutokana na kamati ya maandalizi ya Kombe la Mapinduzi 2026 kupambana kupata wadhamini wengi waliofanikisha zawadi kuongezwa, inatoa chachu kwa ZFF kuboresha zaidi Ligi Kuu Zanzibar kwa kuongeza wadau watakaoifanya ligi hiyo kuwa bora zaidi kama ilivyo mataifa mengine.
“Wadhamini waliopo katika Kombe la Mapinduzi 2026 na zawadi zinazotolewa inatoa hamasa kwa kamati ya maandalizi kuona wakati ujao kuna haja ya kuongeza juhudi ili kuwa bora zaidi ya hapa kwani inawezekana.
“Lakini pia kwetu Shirikisho inatupa kama somo kuona hata ligi ya ndani inajiuza zaidi kwa kuongeza wadau kwani Kombe la Mapinduzi ni mashindano ya muda mfupi, lakini mambo makubwa yamefanyika.
“Sehemu kukiwa na fedha basi mambo mengi yanakwenda ndio maana nikasema hii ni kama changamoto kwetu kuhakikisha mpango wa uendeshaji na usimamizi vinakwenda sawasawa kwa asilimia zote ili hata ligi yetu iwe bora kama wengi wanavyotamani kuwa hivyo ilivyo mataifa mengine,” amesema Kabwanga.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 iliyoanza Desemba 28, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, itahitimishwa Januari 13, 2026 kwa kuchezwa fainali kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.

