Mtoto afa kwa kutumbukia shimoni

Tabora. Mtoto wa miaka mitatu na nusu aitwaye Yasini Sadiki, mkazi wa Kitongoji cha Itetemia, Kata ya Itetemia Manispaa ya Tabora, amefariki dunia baada kutumbukia kwenye shimo lenye maji wakati akicheza na wenzake.

Shimo hilo linalodaiwa kumilikiwa na mchungaji mmoja Tabora Mjini ni maalumu kwa ajili ya kuchimbwa mchanga ambao hutumika kwa ujenzi.

Akizungumzia tukio hilo leo Januari 9, 2026 kamanda wa kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoani Tabora, Loshpay Laizer baada ya kuopoa mwili wa mtoto huyo, amewahimiza wananchi kuwa makini na karibu zaidi na watoto wao hasa kipindi hiki cha mvua ambapo mashimo mengi yamejaa maji.

“Kipindi tulichonacho ni kizuri kwa ajili ya kilimo ili kupata chakula lakini ni kipindi hatari kwenye mazingira yetu hasa maeneo yenye mashimo kama haya ni hatari zaidi kwa watoto na hata watu wazima,” amesema

Ameshauri  wamiliki wa mashimo ya biashara ya mchanga ili kutokua hatarishi kwa wananchi wengine hasa walio jirani na mashimo hayo inakuwa kikwazo kwa michezo ya watoto na hata matumizi ya njia zilizo karibu na mashimo hayo.

“Ni kweli kwamba watu wanafanya biashara ya kuuza hii michanga lakini ni vyema kuwalinda na watumiaji wengine wa ardhi juu ya usalama wao,” ameongeza Loshpay.

Bwawa lililopelekea kifo cha mtoto Yasini Sadiki lililopo kitongoji cha Itetemia manispaa ya Tabora.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Itetemia lilipotokea tukio hilo, Joel Baruti amesema mtoto huyo akicheza na wenzake kando ya shimo hilo alikanyaga ukingoni kwa bahati mbaya akawa ametumbukia hapo ndipo wenzake wakaanza kupiga kelele wakikimbia kuelekea nyumbani kutoa taarifa.

“Kando ya shimo kuna kama njia ambayo watu hua wanapita na kipindi hiki cha mvua kingo za mashimo zinakatika na ndio kilichotokea kwa mtoto Yasini na wakati sasa kwa mmiliki wa shimo kuona namna bora ya kukinga shimo lake,” amesema mwenyekiti

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya majanga na furaha wa kata hiyo Idd Tambwe ameiomba serikali kuhakikisha inadhibiti mashimo yanayopelekea vifo vya watu katika kata hiyo kwa kuwachukulia hatua kali wamiliki wake kwa sababu ni muda mfupi sana tangu kufariki mtoto mwingine kifo cha aina kama hiyo.

Kamanda wa kikosi cha Zimamoto na uokoaji mkoani Tabora Loshpay Laizer akizungumza na wananchi wa Itetemia mara baada ya kuopoa mwili wa mtoto Yasini alitumbukia Bwawani

“Serikali ichukue hatua kali kwa hawa watu wanaochimba mashimo na kuyaacha hovyo kwa sababu yana gharimu maisha ya watu na sio watoto tu na kwamba haina tija kutoa pole kwa wananchi kila mara halafu vifo vya aina hiyo vinajirudia kila siku,” ameomba.

Hamisi Ramadhani mkazi wa Itetemia ambaye pia ni shuhuda wa tukio hilo amesema wakati wanapita njia akiwa na wenzake wakaona watoto wanapiga kelele wanakimbia ndio kusogea eneo hilo na kuona viatu vya mtoto vinaelea kwenye bwawa.

“Sisi tulivyoona kuwa ni mtoto amezama kwenye maji nikampa mwenzangu simu anishikie nikatumbukia kumuokoa mtoto lakini haikuwa bahati yetu maana alikuwa ameshafariki,” amesema.