MCHEZAJI mwenye uwezo wa kucheza safu nzima ya ulinzi na kiungo, Naby Camara amefanya kitu cha kipekee kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inayokwenda kukamilika Januari 13, 2026 kwa kuchezwa fainali kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Camara anayetumia zaidi mguu wa kushoto kusakata kabumbu, hadi kufikia nusu fainali kabla ya jana haijahitimishwa hatua hiyo, alikuwa ndiye mchezaji pekee aliyebeba tuzo mbili tofauti zinazotolewa.
Nyota huyo raia wa Guinea, alianza kubeba Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi, kisha akabeba Tuzo ya Mchezaji Mwenye Mchezo wa Kiungwana ‘Fair Play’.
Tuzo hizo mbili tofauti kila moja imekuwa na zawadi yake ya fedha kutoka kwa wadhamini wa michuano hiyo ambapo Januari 5, 2026 wakati Simba ikishinda 2-1 dhidi ya Fufuni na kufuzu nusu fainali, alitunukiwa Tuzo ya Mchezaji Bora iliyokwenda sambamba na kiasi cha Sh1 milioni.
Baada ya hapo, Januari 8, 2026, Simba ilipochapwa 1-0 na Azam hatua ya nusu fainali na kutupwa nje ya mashindano, ndipo Camara akapewa Tuzo ya Fair Play na Sh1 milioni, kiasi ambacho kimeongezeka kutoka Sh500,000 kilichokuwa kikitolewa hatua ya makundi, huku pia mechi ya fainali kwa mchezaji atakayepewa tuzo hiyo, atakabidhiwa na Sh2 milioni.
Akizungumzia tuzo hizo, Camara ambaye amefunga bao moja katika michuano hiyo, amesema: “Nashukuru kwa mara nyingine tena nimepewa tuzo, kikubwa mimi kama mchezaji nilikuwa natimiza majukumu yangu ndani ya uwanja kuhakikisha Simba inafikia malengo. Kupewa tuzo ni sehemu ya mchezaji kuthaminiwa mchango wake ingawa haijawa upande wetu, tumeshindwa kufikia malengo.”
Wakati Camara akibeba tuzo zote za mashindano hatua ya makundi na nusu fainali, Morice Chukwu anazo tuzo mbili za Mchezaji Bora alizoshinda hatua ya makundi, huku Yakoub Said Mohamed wa Muembe Makumbi akibeba tuzo mbili za Fair Play.
