Ndugu wa mke waliotaka kumdhulumu shemeji nyumba wafukuzwa

Arusha. Wananchi wa Mtaa wa Mashariki, Kata ya Muriet iliyopo Halmashauri ya Jiji la Arusha, wamefanikiwa kuwaondoa baadhi ya ndugu waliokuwa wakitaka kumfukuza shemeji yao baada ya mkewe kufariki dunia.

Michael Mbuya alifiwa na mke wake, Zaiduna Bakari, Desemba 17, 2025 ambaye alizikwa Desemba 20, 2025 jijini Arusha lakini baada ya maziko baadhi ya ndugu wa marehemu waliendelea kukaa kwenye nyumba waliyokuwa wanaishi wanandoa hao huku wakidaiwa kumfukuza shemeji yao na kutaka kwenda kumpangishia chumba sehemu nyingine.

Kutokana na sintofahamu hiyo, juzi, Januari 7, 2026 hali ya taharuki ilizuka katika nyumba hiyo baada ya ndugu hao kuendelea kung’ang’ania kukaa kwenye nyumba hiyo hali iliyowafanya majirani wa Mbuya kuingilia kati na kumsaidia ili asidhulumiwe.

Majirani na Jeshi la Polisi waliingilia kati mgogoro huo kwa siku mbili mfululizo ambapo jana Januari 8, 2026 walifanikiwa kuwaondoa ndugu hao waliodai kuwa nyumba hiyo ni ya dada yao wakati Mbuya anadai nyumba hiyo alijenga na mkewe aliyeishi naye kwa zaidi ya miaka 30.

Akizungumzia kinachoendelea kwenye familia yake, juzi, Mbuya alieleza kuwa ameishi na mkewe kwa zaidi ya miaka 30 ambapo walifunga ndoa Oktoba 23, 2016.

Alidai kuwa mkewe alipata tatizo la kwenye utumbo kuanzia mwaka 2017 ambapo tangu kipindi hicho alikuwa akimuuguza na kuwa walianza kuishi kwenye nyumba za kupanga hadi walipoweza kujenga nyumba hiyo na kuwa katika ndoa yao hawakubahatika kupata mtoto.

“Tulikaa kikao baada ya msiba na kukubaliana kwa sababu sikuwa na mtoto na mke wangu na nikakubali kuchukua baadhi ya familia yake. Ila wamekuja kunigeuka wanasema sina haki kwenye nyumba hii,” alisema.

Mbuya alidai kuwa ndugu hao wa mkewe walimweleza kuwa wameenda kumpangishia chumba kimoja cha kuishi eneo la Kwa Morombo na kumtaka aondoke kwenye nyumba hiyo.

“Wanataka niondoke wanadai wamenipangishia chumba niondoke sina haki ya kuishi hapa, wakati nimejenga na mke wangu. Nashangaa baada ya kuzika, familia hii haitaki kuondoka wanataka mimi ndiyo niondoke niwaachie nyumba, wanasema sina haki kwenye hii nyumba, mwisho wakaniambia nimehusika kumuua mke wangu,” amesema.

Jana, baada ya ndugu hao kuondoka, Mbuya aliwashukuru majirani zake kwa kumsaidia kwani bila wao asingeweza kuwaondoa watu hao.

“Nashukuru sana majirani zangu kwa hiki mlichonisaidia kwa kuwaondoa watu hawa, Mungu awabariki sana kwani shughuli ilikuwa ngumu peke yangu nisingeweza,” amesema.

Awali, baadhi ya majirani wa Mbuya walieleza kushangazwa na baadhi ya ndugu hao kung’ang’ania kukaa kwenye nyumba hiyo na kuwa waliamua kuingilia kati ili mume huyo asikose haki yake kwa kudhuliwa nyumba hiyo.

Mmoja wa majirani hao, Sekunda Kimario amedai kuwa wanamfahamu Mbuya na marehemu mkewe na kuwa wameamua kusimama kama majirani kumtetea ili apate haki yake.

“Huyu baba ni jirani yetu na tunampenda sana, alipata matatizo akafiwa na mkewe sasa tangu hao ndugu wa mke wang’ang’anie hapa ameanza kutembea barabarani anaongea mwenyewe, tukaona kama wananchi tumsaidie ndiyo maana tumeamua kusimama kumtetea.

“Tangu nihamie huu Mtaa, mwaka 2020, alikuwa akiishi na mkewe vizuri, ndugu wamekuja kuingia tamaa kwa sababu wanaona hawa wanandoa hawakubahatika kupata watoto, wakaona wamdhulumu mzee,” amesema na kuongeza:

“Sisi kama wananchi hatutaki kuona mwenzetu anaonewa, sisi kama majirani tunaomba na huyu baba apewe ulinzi na hatutaki kuwaona katika eneo hili, tuko hapa kutetea haki za huyu baba,” amesema.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo, Jonathan Philemon amesema walipata taarifa hizo na kuwa wao walishauri kama wanaona nyumba ni haki yao, wafuate taratibu za kisheria.

“Ni sahihi hawa waliokuwa kwenye nyumba kumpisha Mbuya na kama kuna haki yao kwenye hiyi nyumba wafuate taratibu za kisheria ili wapate haki yao ikibainika huyu baba si mhusika, niwaombe wananchi msifanye fujo,”

Mjumbe mwingine wa mtaa huo, Halima Shaban amesema kuwa jambo hilo siyo zuri kwa sababu mke akifa siyo vizuri mumewe kufukuzwa kwenye nyumba.

Mwananchi mwingine katika mtaa huo, Joseph Alex, amesema wanashukuru kwa hilo walilolianzisha jana na kufanikiwa kumsaidia Mbuya asiondolewe kwenye nyumba hiyo.

“Ulinzi tutaimarisha na hatutakubali kuona upuuzi kama huu, sisi majirani tutaendelea na ushirikiano na kupambana kuhakikisha hakuna anayeonewa,” amesema.

“Tunashukuru tumeondoa wavamizi na baada ya kuondoka amani imerejea katika mtaa na hili linatukumbusha kuwa ujirani ni bora zaidi, umoja huu umeonekana kuanzia jana na inaonyesha kuwa jirani ni ndugu wa kwanza hata kama hamjashea damu, ukiua ujirani umeya nasaba yako ya kweli ambayo utakulindwa,” amesema.

Mmoja wa ndugu wa Mbuya, Israel Kombe amewashukuru majirani kwa umoja na ushirikiano huo uliomsaidia ndugu yao kubaki kwenye nyumba yake.

“Tunashukuru sana majirani kwa umoja wenu asanteni mmepoteza muda wenu mwingi na huu ushirikiano mliofanua ni mzuri Mungu awatunze muendelee na umoja huu tulikuwa mbali tumekuja na tumeshngaa ila tunashukuru majirani mmefanya imekuwa hivi” amesema.