UONGOZI wa Namungo uko katika hatua za mwisho za kuipata saini ya beki wa kati wa Azam FC, Ali Hassan Chamulungu kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu, baada ya mazungumzo chanya kati ya pande mbili, ili nyota huyo apate nafasi zaidi ya kucheza.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Namungo, umeliambia Mwanaspoti mazungumzo na Azam ya kumpata beki huyo yamefikia sehemu nzuri, kwa lengo la kwenda kuboresha eneo hilo, baada ya kuondoka Mghana Daniel Amoah, aliyemaliza mkataba wake.
“Chamulungu ni miongoni mwa wachezaji wa Azam watakaotolewa kwa mkopo dirisha hili ili wakapate nafasi ya kucheza sehemu nyingine, sisi tumeiona pia hiyo fursa na sasa tumefungua mazungumzo ili kumpata kikosini kwetu,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumzia suala hilo, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman, amesema baada ya kupokea ripoti ya benchi la ufundi tayari wameanza kuangalia maeneo ya kuongezea nguvu, ambapo muda wowote kuanzia sasa watatangaza wachezaji wapya waliowasajili.
“Kila timu kwa sasa iko sokoni na hatuwezi kusema tunamtaka mchezaji huyu au yule kwa sababu kwa kufanya hivyo, unazidi kufungua wigo mpana na wengine kuingilia kati, tunaboresha kwa siri kubwa ila kwa kuzingatia pia malengo,” amesema Ally.
Beki huyo ambaye ni nahodha wa timu ya vijana ya Azam chini ya miaka 20, alisaini mkataba wa kuichezea klabu ya wakubwa Julai 24, 2025 wa hadi mwaka 2030.
