Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam limewakamata watu wanne wanaoendelea kuhojiwa kwa tuhuma za unyang’anyi, kujeruhi na kupora watu barabarani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Januari 8, 2026 iliyotolewa na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro tukio hilo limetokea Januari 8, 2026 saa 8:40 mchana maeneo ya Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni, eneo la Mwendokasi.
“Inadaiwa kundi la watu, wengi wao wakiwa wamepanda pikipiki na baadhi wakiwa na mapanga, walifanya vitendo vya unyang’anyi na uporaji huku wakiwa na jeneza la marehemu aliyefahamika kwa jina la Ibrahimu Elia, mkazi wa Mabwepande,” amesema Kamanda Muliro.
Amesema marehemu Elia anadaiwa kuuawa Januari 2, 2026 maeneo ya Bunju baada ya kushambuliwa na kundi la wananchi waliomtuhumu kujihusisha na uporaji wa pikipiki katika maeneo ya Goba.
Katika tukio hilo, watu wanne waliripotiwa kuporwa mali zao na wengine kujeruhiwa. Walioathirika ni Japhet Kalanga (41), mfanyabiashara mkazi wa Mabwepande, ambaye amejeruhiwa kichwani na kuporwa simu.
Kamanda Muliro amesema mwingine aliyekutwa na kadhia hiyo ni Joshua Leguna (26), mkazi wa Mabwepande, amejeruhiwa puani na mkono wa kulia, kuporwa simu pamoja na fedha taslimu Sh20,000.
Naye, Mhandisi wa Hospitali ya Mabwepande, Abas Mdoe (34), ameporwa simu na Sh1 milioni huku Maria Lameck (28), mfanyabiashara mkazi wa Mabwepande, akiporwa simu na Sh100,000.
Hata hivyo, amesema Jeshi la Polisi lilifanikiwa kudhibiti hali hiyo haraka baada ya kulazimika kufyatua risasi hewani, hatua iliyowezesha kukamatwa kwa baadhi ya watuhumiwa.
“Baada ya hali kutengemaa, ndugu wa marehemu waliendelea na taratibu za mazishi na marehemu alizikwa katika makaburi ya Mabwepande, hali ya usalama ikirejea kuwa shwari,” amesema Muliro.
Jeshi la Polisi limewakumbusha wananchi kuendelea kutii sheria za nchi, likisisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayekiuka.