PPP CENTRE YAELIMISHA WADAU KUHUSU MIRADI YA UBIA NCHINI

KITUO cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ( PPP Centre), kimeendesha mafunzo kwa wafanyabiashara, wawekezaji na maafisa kutoka taasisi za kiserikali katika Halmashauri za Mkoa wa Tanga, kikielimisha juu ya kazi zinazofanywa na kituo hicho.

Akizungumza kwenye kikao kazi kilichofanyika mwishoni mwa wiki mkoani Tanga, kikihusisha makundi hayo, Mkuu wa Kitengo cha Uchambuzi/Tathmini wa Miradi, katika Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-Centre), nchini Tanzania Dkt. Suleiman Kiula, amesema miongoni mwa kazi zinazofanywa na kituo hicho ni pamoja na kusimamia nakuendeleza miradi ya ubia nchini.

Pia Kiula, ameeezea umuhimu wa kutumia PPP katika utekelezaji wa mipango ya Taifa kwa maendeleo ya nchi, muundo wa kisheria na kitaasisi katika katika utekelezaji wa program ya PPP nchini.

“Kuna wakati Serikali inaweza ikaanzisha miradi lakini katika kuisimamia inaweza kuwa changamoto kidogo, hivyo kwa umuhimu huo Serikali ikaanzisha sera ya ubia kwa kutumia sekta binafsi ifanye jukumu lake”, amesema Kiula.

Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi Mradi wa HEET Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lihoya Chamwali ameipongeza PPP-Centre kwa kazi nzuri inayoendelea kufanya katika kuhakikisha inasimamia miradi ya maendeleo, huku akisema kuwa bado chuo hicho kinaendeleo na ujenzi wa jengo katika chuo hicho ambao utakamilika mwezi Machi mwaka huu.