Shinyanga. Wakazi wa Kata za Ndala, Masekelo, Mwawaza na Mjini katika Manispaa ya Shinyanga wamelalamikia kusuasua kwa ujenzi wa barabara ya Mwawaza inayoelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, wakisema unawasababishia usumbufu wanapowapeleka wagonjwa hospitalini.
Wakizungumza leo Ijumaa Januari 9, 2026 wakati wa ukaguzi wa ujenzi huo, wakazi wamesema barabara hiyo imekuwa hatarishi, hasa katika kipindi hiki cha mvua, huku wengine wakishindwa kuvuka kwenda upande wa pili kwa usalama.
Mmoja wa wakazi hao, Paulo Mahendeka amesema kuchelewa kukamilika kwa ujenzi huo kumegeuka kuwa kero ya kila siku kwa wananchi, hususan kwa huduma za dharura.
“Kwa sasa tunaona magari yakibeba mchanga kuendelea na ujenzi, lakini bado hali ni mbaya. Wagonjwa wanachelewa kufika hospitalini na maisha yanakuwa hatarini,” amesema.
Diwani wa Kata ya Ndala, Zamda Shabani, amesema mkandarasi aliondoa vifaa vyake vyote eneo la mradi kabla ya sikukuu za Desemba 2025, hatua iliyosababisha kazi kusimama kwa muda mrefu na kuzua sintofahamu miongoni mwa wananchi.
Amesema barabara mbadala inayotumika kwa sasa ni nyembamba na isiyo salama, hali inayoongeza kero kwa watumiaji wa njia hiyo.
Kwa upande wake, Mhandisi mshauri kutoka Kampuni ya Mshauri Consultant, Alfred Kameya amesema mkandarasi yuko nyuma kwa utekelezaji wa mradi kwa takribani asilimia 30, licha ya kuwa tayari amelipwa fedha kwa kazi hiyo.
Ameeleza kuwa mkandarasi tayari ametumia miezi sita sawa na asilimia 40 ya muda wa mkataba, huku miezi tisa iliyobaki ikiwa ni asilimia 60 ya muda wote wa utekelezaji wa miradi miwili.
Naye mkandarasi kutoka Kampuni ya Sihotech, Edward Rwezahura amesema mvua zinazoendelea kunyesha zimekuwa changamoto katika utekelezaji wa baadhi ya kazi za ujenzi, hali iliyochangia kusuasua kwa maendeleo ya mradi.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita ametoa maagizo kwa mkandarasi kuhakikisha anatekeleza miradi yote kwa mujibu wa mkataba, ikiwemo ujenzi wa stendi kuu ya mabasi ya mkoa na barabara ya lami inayoelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mhita amesema hana sababu ya kukubali visingizio vya kuhamisha nguvu kazi kutoka mradi mmoja kwenda mwingine, akisisitiza mkandarasi alipaswa kujiridhisha kuhusu uwezo wake kabla ya kuomba zabuni.
“Kilicho muhimu ni miradi ikamilike ndani ya muda uliopangwa,” amesema.
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ilisaini mkataba wa Sh26 bilioni na Kampuni ya Sihotech kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji (Tactics), unaohusisha ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi ya mkoa katika Kata ya Kizumbi pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 5.8 inayoelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mradi huo ulianza Julai 15, 2025 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 14, 2026, ingawa hadi sasa uko nyuma kwa utekelezaji wa takribani asilimia 30.
