Serikali kuongeza eneo la malisho ya mifugo

Tabora. Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi inaongeza maeneo maalumu ya malisho kwa ajili ya mifugo kutoka hekta milioni 3.4 zilizokuwapo hadi kufikia hekta milioni sita ifikapo mwaka 2030.

Hatua hiyo ni pamoja na kuzalisha mbegu za kisasa za malisho ambazo zitauzwa kwa bei ya ruzuku ya Sh1,000 kwa kilo moja kutoka Sh4,000, mpango unaotarajiwa kuongeza tija katika sekta ya ufugaji nchini.

Hayo yamejiri wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani katika wilaya za Nzega na Igunga, mkoani Tabora iliyolenga kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji mkoani hapa.

Amesema uamuzi wa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi umekuja wakati huu ili kuleta suluhu ya uhaba wa maeneo ya malisho ya mifugo nchini, ukiwemo Mkoa wa Tabora.

Amesema mifugo inapaswa kupata malisho ya kutosha ili iweze kuwa na afya nzuri.

“Tumeshaona kwamba watu wanaendelea na ufugaji kwa kasi kubwa, ni lazima Serikali  ione namna bora ya kuwezesha malisho ya mifugo hiyo na hata mbegu tunawapa kwa ruzuku ili kuwa na uhakika zaidi wa malisho,” amesema.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Damas akizungumza na wafugaji mkoani Tabora katika ziara yake mkoani humo iliyolenga kuongeza maeneo ya malisho.

Amesema halmashauri zote zinazoguswa na mpango huo zinapaswa kuanza kutenga maeneo, zikiwamo zote za Mkoa wa Tabora ambao kwa asilimia 95 eneo lake ni misitu.

Baadhi ya misitu hiyo ni ya hifadhi na mingine ina wanyama hivyo eneo la shughuli za kibinadamu ni dogo.

“Tabora hapa eneo kubwa ni hifadhi kwa hiyo sehemu ambayo wanaishi watu pamoja na kufanya shughuli zao ni dogo, ndiyo maana Serikali imekuja na mpango huu ili kupata suluhu ya changamoto hiyo,” amesema.

Mwenyekiti wa wafugaji Mkoa wa Tabora, Simon Butili, amesema eneo la malisho ni changamoto kubwa, kwani hata wakati wa mvua za masika majani yanakua mengi lakini eneo linaloruhusiwa kwa uchungaji mifugo ni dogo, hivyo afya ya mifugo haiimariki na wakati wa ukame hufa.

“Serikali imeamua hatua nzuri na bora kwetu, tukipata malisho ya kutosha mifugo itakua mizuri lakini hata soko lake litapanda kwani ng’ombe mwenye afya nzuri bei yake pia ni kubwa zaidi na sisi wafugaji tunanufaika,” amesema.

Mwenyekiti wa wafugaji Mkoa wa Tabora, Simon Butili akiwasilisha changamoto za wafugaji mkoani Tabora mbele ya naibu waziri wa mifugo na uvuvi.

Shija Masanja, mfugaji wilayani Nzega, amesema hatua ya kuongeza malisho kwa ajili ya mifugo itatatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

“Ni hatua muhimu kwetu sisi kwani tukiangalia maisha yetu yanategemea zaidi kilimo na ufugaji,” amesema.