Simba yamvutia waya Sillah | Mwanaspoti

SIKU chache baada ya Mwanaspoti kuripoti aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Gibril Sillah, amevunja mkataba na ES Setif ya Algeria, uongozi wa Simba umemvutia waya ili aweze kurudi Ligi Kuu Bara.

Nyota huyo alijiunga na kikosi hicho na kusaini mkataba wa hadi Juni 30, 2027, ingawa makubaliano ya kuusitisha yamefikiwa, huku ikidaiwa sababu kuu zilizochangia ni kutolipwa mshahara kwa miezi minne na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kililiambia Mwanaspoti, wanatamani kupata saini ya Sillah baada ya kuvunja mkataba alikokuwa, kwani wanaamini wanakosa aina ya uchezaji kama wake kikosini mwao sasa.

“Hatuna kiungo bora aina ya Sillah ambaye tayari ameonyesha ubora ndani ya Azam FC kabla ya kutimka Algeria, ni mchezaji tulijaribu kumtaka kabla lakini tulikwama kutokana na ofa kubwa aliyoipata,” kimesema chanzo hicho.

SILL 01

Simba inamzivia Sillah kutokana na wachezaji wanaocheza nafasi hiyo kwa sasa klabu, Elie Mpanzu na Jean Charles Ahoua, wakitajwa kuwa mguu ndani mguu nje klabuni licha ya kuwa na mikataba na Simba na anatajwa kama anayeweza kuziba mashimo haraka kwa uwezo alionao.

Mwanaspoti lilimsaka Sillah na kumuuliza juu ya mipango yake na kusema kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba na waajiri wake wa zamani kwa sababu mbalimbali huku akiweka wazi kuwa amefanya uamuzi sahihi.

“Ni kweli nimevunja mkataba kwa makubaliano maalum na waliokuwa waajiri wangu kwangu ni uamuzi sahihi sijutii na nimefanya hivyo kipindi sahihi cha dirisha la usajili ninachokiangalia sasa ni kupata timu ambayo itanipa nafasi ya kucheza mara kwa mara,” amesema Sillah na kuongeza;

SILL 02

“Ofa ni nyingi lakini nataka kupata muda wa kufanya chaguo sahihi ni timu gani naenda na inashiriki mashindano gani ushindani wa ligi yao na mambo mengine muhimu nje ya uwanja ambayo yatanifanya nipambane.”

Mwanaspoti lilipomuuliza ofa alizonazo kwa hapa nchini alijibu kwa kifupi kuwa kuna timu moja kutoka Ligi Kuu ambayo imeonyesha nia ya kumhitaji na anaheshimu soka la Tanzania ambalo amelitaja kuwa ni la ushindani na linakua msimu hadi msimu.

“Nimepigiwa na mmoja wa viongozi kutoka Tanzania kuwa bado wana nafasi ya kusajili na wana uhitaji wa mchezaji wa aina yangu, bado hatujamalizana ila nilimuambia nitamrudia anatakiwa kunipa muda ili niweze kufanya uamuzi.”

Kiungo huyo aliyehusika na mabao 13 ya Ligi Kuu 2024-2025 akiwa na Azam baada ya kufunga mabao 11 na kuasisti mawili, kwa 2025-2026 ameasisti mabao matano katika mechi 13 za mashindano yote alizoichezea ES Setif.