Russia. Heri ya sikukuu ya Mwaka Mpya 2026, ndugu wasomaji. Katika kuupokea mwaka huu, leo nitawapa dondoo za kiafya ambazo ukizizingatia, zitakuwezesha kuishi kwa afya njema na kufanya mwaka huu kuwa bora zaidi kwako.
Kwanza kabisa, fahamu kwamba sera ya bima ya afya ya Taifa kwa wote inakuja mwaka huu. Pindi itakapokuwa tayari, hakikisha unajiunga nayo. Bima ya afya ni muhimu sio tu kwako, bali pia kwa familia na jamii yako.
Pili, mojawapo ya malengo yako kwa mwaka huu iwe kujua hali ya afya yako. Jenga tabia ya kupima afya angalau mara mbili kwa mwaka. Ukishindwa mara mbili, hata mara moja si mbaya; hatua yoyote ni bora kuliko kutofanya kabisa.
Tatu, mojawapo ya changamoto kubwa za kiafya hapa nchini ni magonjwa yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya moyo na mishipa, kisukari, ugonjwa sugu wa figo, kiharusi na saratani.
Magonjwa haya yanazuilika kwa kuepuka mitindo mibaya ya maisha, ikiwemo ulaji holela, kutofanya mazoezi, ulevi na matumizi ya tumbaku.
Nne, unene uliokithiri ni tatizo linalohatarisha afya na kuongezea hatari ya magonjwa yasiyoambukiza. Dhibiti ulaji holela na fanya mazoezi mara kwa mara ili kudumisha uzito unaofaa.
Tano, kufanya mazoezi na kushughulisha mwili mara kwa mara husaidia kujikinga na magonjwa mengi. Utamaduni wa mazoezi uanzie nyumbani, ili wazazi wawe mfano mzuri na kuwajengea watoto tabia ya kupenda mazoezi. Kwa mujibu was Shirika la Afya Duniani (WHO), kufanya mazoezi angalau dakika 150 kwa wiki kunatoa matokeo chanya kiafya.
Sita, Matukio ya wagonjwa wa akili wakiwamo wanaosumbuliwa na msongo wa mawazo, sonona, hofu kali na kujiua yameripotiwa kuongezeka mwaka jana.
Jikinge kwa kuepuka shinikizo la akili na kuzingatia ishara za tahadhari kama msongo wa mawazo, kukosa usingizi, kujitenga, hasira zisizo na sababu, mawazo ya kujiua, au kusikia sauti zisizoeleweka. Fika mapema katika huduma za afya unaposhuhudia dalili hizi.
Saba, hakikisha unapata burudani, pumzika na usingizi bora angalau saa 8-10 kwa usiku. Ukikosa usingizi wa kutosha, hakikisha unapata msaada wa kitaalamu.
Ubora wa usingizi huimarishwa kwa kudumisha muda wa kulala, kulala mahali tulivu, penye baridi na giza, na kuepuka mitandao ya kijamii, vipindi vya kusisimua, na chakula kabla ya kulala.
Nane, tumia angalau dakika 15 kila siku kuwa peke yako, sali, waza mawazo chanya, vuta hisia nzuri, na jenga ujuzi mpya. Hii inasaidia kupunguza mkazo wa akili na kuboresha utendaji wa mfumo wa fahamu.
Tisa, changamana na jamii. Kuwa rafiki wa mazingira unayoishi, zingatia usafi, tunza mazingira na zingatia kanuni za afya. Simu janja inaweza kuwa chachu ya afya njema au mbaya. Dhibiti matumizi yasiyo na tija na pakua aplikesheni zinazotambulika za ushauri wa afya.
Kumi, matukio ya ajali za barabarani mwaka jana yamesababisha vifo vingi na ulemavu wa kudumu. Timiza wajibu wako ukiwa mtembea kwa mguu, dereva, au abiria kwa kuzingatia sheria za barabarani.
Mwisho, fahamu kuwa si kila mwenye koti jeupe ni daktari. Tambua anayekuhudumia, fahamu kituo cha afya unachopata huduma, na jua haki na wajibu wako.
Usinunue dawa, vipodozi, au virutubisho mtandaoni au kwa watu wasiotambulika.
Kwa kufuata dondoo hizi, unaweza kuanza mwaka mpya ukiwa na afya bora, akili timamu, na matumaini chanya ya maisha.
