UCHAMBUZI WA MJEMA: Simbachawene alivyoshika na kuuishi wosia wa Mzee Mwinyi

Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili (1985-1995), Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema maisha ya mwanadamu hapa ulimwenguni ni hadithi tu, nami naona George Simbachawene ameushika na kuuishi wosia huu akiwa hai hapa duniani.

Ndio maana leo hii, licha ya kutenguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu ambazo wala Rais hawajibiki kusema, anazungumzwa vizuri katika kila kona ya nchi kwamba aliitendea haki nafasi yake ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Ni lazima hapa niseme mapema kuwa ibara ya 36(1) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 imempa Rais mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Katiba hiyo hiyo Ibara ndogo ya (2) na (3) inasema Rais anayo mamlaka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi, lakini pia ana mamlaka ya kuwapandisha vyeo, kuwaondoa katika madaraka na kuwafuta kazi watu hao.

Kwa hiyo tutakuwa hatumtendei haki Rais kuhoji kwa nini anamteua huyu au kumtengua wakati hayo ni mamlaka yake ya kikatiba na Ibara ya 37(1) inasema atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote.

Mie ninaona, sisi ambao tunaiweka Serikali madarakani kwa mujibu wa Katiba, tuna haki ya kutoa maoni yetu kama Ibara ya 18(1) ilivyotupa mamlaka hayo, kuyatumia kupima utendaji kazi, mwenendo na tabia ya wale wanaoteuliwa.

Siku zote na ama mara nyingi, Rais anapowaapisha wale aliowateua hugusia sababu za kwanini amemteua, na mara chache sana kusema kwanini alimtengua mtangulizi wake, na hata asiposema hiyo haitazuia wananchi kuweka hisia zao.

Hasa ikizingatiwa kuwa Simbachawene aliteuliwa kuwa Waziri Novemba 17,2025 na jana Januari 8,2026 ametenguliwa, hii akiwa amehudumu kwa siku 52 tu, kwa mwanadamu yeyote anayefikiri sawa sawa lazima ahisi kuna tatizo mahali.

Kama nilivyotangulia kumnukuu Mwinyi, maisha ya mwanadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni, kila mtu anapaswa kuwa hadithi nzuri kwa hao watakaosimuliwa (akitangulia), Simbachawene tayari ameitengeneza akiwa hai.

Simbachawene aliteuliwa kushika wadhifa wa waziri wa mambo ya ndani ya nchi katika kipindi ambacho ndio kwanza nchi iko kwenye mtikisiko wa yale yaliyofanywa na vyombo vya usalama Oktoba 29 na siku kadhaa zilizofuata.

Hakuna ubishi siku hiyo ya uchaguzi kulitokea vurugu zilizosababisha vifo vya watanzania wetu, majeruhi na mali kuharibiwa na ndio maana Rais Samia kwa kutambua ukubwa wa tatizo, aliamua kuunda Tume ya uchunguzi wa yaliyotokea.

Matokeo ya Tume hiyo ndio ambayo yatamfanya Rais sasa aende hatua ya pili ya kuanzisha maridhiano ili kulirudisha taifa pamoja, kuwawajibisha waliohusika na matendo yale mabaya ambayo yamepewa jina la kuzima “uasi” nchini.

Huwa mara nyingi nasema ukweli huwa una sifa moja kuu, kwamba ukiukataa haugeuki kuwa uongo, kwamba matukio hayo yameibua chuki za wananchi walio wengi, dhidi ya Serikali na viongozi wake na hasa hasa Jeshi la Polisi.

Kabla ya matukio hayo yaliyoanzia Oktoba 29, tayari nchi yetu ilikuwa katika giza nene na sintofahamu kutokana na ukamataji holela unaofanywa na baadhi ya Polisi, utekaji, kupotea kwa watu na mauaji ya baadhi ya waliotekwa.

Sasa katika kipindi kifupi cha uongozi wake, Simbachawene alianza kutibu majeraha na kujaribu kurejesha imani ya wananchi kwa Serikali na Jeshi la Polisi, lakini ghafla tu anatenguliwa, tayari wananchi wana majibu kichwani mwao.

Tumemsikia na kumuona Simbachawene akikemea aina ya ukamataji uliokuwa unafanywa na Polisi (ambao umeibua chuki kubwa), akisema ameshamwelekeza Inspekta Jenerali (IGP), Camilius Wambura kuwa hataki aina hiyo ya ukamataji.

Simbachawene akasema ukamataji ule anaupenda ni ule kwa mujibu wa sheria, ambapo askari amevaa sare, anashirikisha uongozi wa mtaa au kijiji, anajitambulisha na mshukiwa anajulishwa kosa na anapelekwa kituo gani.

Tena akaenda mbali na kusema tena wakati mwingine mtu anayekwenda kukamatwa anajulikana, biashara zake zinajulikana na ofisi zake zinajulikana, kwanini polisi waende usiku wa manane tena wakiwa wamevaa kininja.

Simbachawene akasema amekubaliana na IGP kwamba ukamataji huo hapana, bali warudi kwenye ukamataji wa staha ambao wananchi wameuzoea badala ya ukamataji unaotisha hadi watoto nyumbani na kuacha kumbukumbu mbaya.

Lakini akakemea pia kwamba mtu amechapisha kitu kidogo tu mtandaoni, anashitakiwa kwa uchochezi jambo ambalo limeibua chuki kubwa kati ya polisi na raia hasa ikizingatiwa kuwa Katiba ya nchi inatoa haki ya uhuru wa mawazo.

Katika video mbalimbali zilizopo kwenye hifadhi ya umma (public domain), Simbachawene alionekana akitekeleza kwa vitendo mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais, pale alipoeleza kulifumua Jeshi la Polisi.

Mbali na video hizo, Simbachawene amesikika akizungumzia neno haki haki haki kwa raia, neno ambalo linaonekana ni gumu kwa baadhi ya viongozi wetu lakini yeye hakuona soni kuhubiri kuhusu haki kwamba ndio msingi wa amani.

Ukisoma ripoti ya Tume ya Haki Jinai na mapendekezo yake, katika kifungu cha 3.1.1 inasema wazi taswira ya Jeshi la Polisi kwa wananchi imechafuka.

Hii ni kutokana na malalamiko ya kushindwa kuzuia uhalifu, matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia kesi, vitendo vya rushwa, mali za watuhumiwa kupotea vituoni na kuchelewa kufika kwenye maeneo ya matukio.

Hali hiyo inasababisha wananchi kupoteza imani kwa Jeshi la Polisi na kutokutoa ushirikiano unaotakiwa na ikapendekeza pamoja na mambo mengine, kwamba Polisi libadilishwe kisheria, kimuundo na kifikra na kuwa Huduma Polisi Tanzania.

Kubadilisha mitaala ya mafunzo na mtazamo wa askari wa Jeshi la Polisi ili kutoka katika dhana ya ujeshi kwenda dhana ya kuhudumia wananchi (police service).

Ukisoma kifungu cha 2.2 tume ilibaini kuwa, vyombo vyenye mamlaka ya kukamata likiwamo Jeshi letu la Polisi, mara nyingi hutumia nguvu kubwa kupita kiasi na kusababisha mateso kwa watuhumiwa.

Lakini uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka ya kukamata pia umelalamikiwa na wananchi kuwa inakuwa vigumu kutambua taasisi iliyomkamata ndugu yao na mahali alipohifadhiwa.

Aidha, tume ikabaini kuwa uwepo wa vyombo vingi vya ukamataji na vyenye mahabusu umetafsiriwa na jamii kuwa ni sababu mojawapo ya watu waliokamatwa kupotea wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola.

Haya ndio mambo ambayo Simbachawene alisimama kuyakataa na akitaka Jeshi la Polisi lifanyiwe mabadiliko makubwa, lakini ndio huyo ametenguliwa na kutenguliwa kwake kunaibua maswali mengi, watawala walitaka afanye nini?

Ndio maana mimi na naamini na Watanzania walio wengi, hata kwa kupitia katika mitandao ya kijamii, wanaona Simbachawene hana deni nao, kazi ameifanya na ameweka hadithi nzuri ambayo vizazi vitasimuliwa atakapoondoka duniani.

Inawezekana ameteleza mahali, nasema inawezekana kwa sababu hiyo ni siri ya mtungi, lakini mimi na baadhi ya Watanzania tulio wengi tunaona Simbachawene ameitendea haki nafasi aliyopewa japo amehudumu kwa siku 52 tu.

Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 065660090