Utenguzi wa Simbachawene wageuka gumzo

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene zikiwa zimepita siku 52 tangu alipotangaza baraza jipya la mawaziri, Novemba 17, 2025, suala ambalo licha ya kuwa ndani ya mamlaka ya mteuaji, limeibua gumzo likihusishwa na matukio na kauli zake za hivi karibuni.

Simbachawene anakuwa waziri wa kwanza kutenguliwa kwenye Baraza la Mawaziri alilolinda baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Januari 8, 2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, Rais Samia amemteua Patrobas Katambi kuwa waziri katika wizara hiyo, akichukua nafasi ya Simbachawene ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Kabla ya uteuzi huo, Katambi alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, sasa amepandishwa cheo na kuwa waziri kamili, akiaminiwa kwenda kuisimamia wizara hiyo nyeti inayosimamia vyombo vya usalama kama Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji.

Mbali na uteuzi huo, Rais Samia amemteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalumu). Kabla ya uteuzi huu, Profesa Kabudi alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Wakati huohuo, Rais Samia amemteua Paul Makonda kuwa Waziri wa Kabla ya uteuzi huu, Profesa Kabudi alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Makonda alikuwa Naibu Waziri katika wizara hiyo.

Kwa upande wa naibu mawaziri, Rais Samia amemteua Dennis Londo kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara akitoka kwenye nafasi hiyo katika Wizara ya Mambo ya Ndani. Vilevile, amemteua Ayoub Mohamed Mahmoud kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani.

Tangu ameteuliwa kuongoza wizara hiyo, Simbachawene amekuwa akizungumzia mabadiliko katika Jeshi la Polisi akilitaka kufanya kazi kwa weledi ili kuondoa malalamiko ya wananchi ambao wanadai kunyanyaswa na askari na kusababisha uhusiano mbaya baina ya pande hizo, kauli ambazo zimesambaa kwa kasi baada ya uteuzi wake kutenguliwa.

Akizungumza na vyombo vya habari, Desemba 8, 2025, kuhusu maandamano yaliyopangwa kufanyika Desemba 9, 2025, Simbachawene alisema ameelekezwa na Rais kwamba afanye kazi kurejesha uhusiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi.

Alisisitiza kwamba lazima mabadiliko yafanyike ikiwemo mabadiliko ya kimfumo na kiutashi. Alisema lazima wakayaangalie mafunzo yanayotolewa kwa askari, kwamba wanakwenda kupambana na wananchi au kuwalinda.

Vilevile, alisisitiza kuyafanyia kazi mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kwamba kuna haja ya kwenda kuyafanyia kazi hususani kulifanya jeshi kuwa la kutoa huduma kwa wananchi badala ya kutumia nguvu.

Katika hatua nyingine, Simbachawene alisikika akizungumzia ukamataji unaofanywa na Jeshi la Polisi, akisisitiza kwamba hakuna haja ya jeshi hilo kutumia nguvu kubwa, kwenda na silaha kumkamata mtu aliyetenda kosa dogo kama kutoa maoni kwenye mtandao.

Anapendelea ukamataji kwa mujibu wa sheria kwamba askari anakwenda akiwa amevaa sare, anaripoti kwa mjumbe kwamba anamhitaji fulani kwa ajili ya mahojiano, basi anachukuliwa tena mchana kwani anafahamika katika eneo husika.

Wiki mbili zilizopita, Simbachawene alishiriki ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, ambako alisema maridhiano ya kweli si suala la siku moja, bali ni mchakato unaohitaji uvumilivu, ustahimilivu, unyenyekevu na ushirikiano wa wadau wote.

Alisisitiza kwamba Serikali iko tayari kusikiliza, kujifunza na kurekebisha pale inapobidi kwa lengo la kulinda umoja na mshikamano wa Taifa.

Alimhakikishia Askofu wa dayosisi hiyo, Dk Benson Bagonza kwamba Serikali itaendelea kuthamini sauti yake na viongozi wengine wa kiroho kama washirika muhimu katika ujenzi wa taifa lenye haki, amani.

Simbachawene ni mmoja wa mawaziri wakongwe katika Serikali ambao wametumikia katika wizara tofauti na kwa nyakati tofauti katika awamu ya nne, tano na sita kabla ya uteuzi wake kutenguliwa.

Amekuwa ni waziri ‘kiraka’ kwa sababu amekuwa akihamishiwa katika wizara tofauti pale yanapofanyika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na yeye akiendelea kuwa sehemu ya mawaziri wanaopewa tena nafasi.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Novemba 17, 2025, alikuwa Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Kabla ya hapo, Januari 2022, katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Samia, alipelekwa Wizara ya Katiba na Sheria na badaye Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Baada ya kushinda ubunge mwaka 2010, Simbachawene aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini kuanzia Mei 2012 hadi Januari 2014 alipohamishiwa Wizara ya Nyumba na Makazi akiendelea kuwa naibu waziri.

Januari 2015 alipandishwa cheo na kuwa Waziri wa Nishati na Madini akichukua nafasi ya Profesa Sospeter Muhongo aliyejiuzulu kutokana na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.

Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015 na kutangaza baraza lake la mawaziri, Simbachawene aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) hadi mwaka 2017 alipojiuzulu kufuatia maelekezo ya Rais Magufuli.

Julai 21, 2019, Rais Magufuli alimteua tena Simbachawene kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira akichukua nafasi ya January Makamba ambaye uteuzi wake ulitenguliwa Januari 23, 2020.

Baadaye Januari 23, 2020, Simbachawene aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya ndani kuchukua nafasi ya Kangi Lugola ambaye naye uteuzi wake ulitenguliwa.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Denis Konga amesema kuondolewa kwa Simbachawene kumeibua mjadala katika jamii kutokana na uongozi wake ulivyokuwa ukibeba matamanio ya wananchi wengi, hasa kuhusu usimamizi wa Jeshi la Polisi nchini.

“Huu mjadala unaoendelea kuhusu kutenguliwa kwa Simbachawene kwa kiasi kikubwa unatokana na sauti yake, hasa kuhusu marekebisho ya kurudisha Jeshi la Polisi kuwa taasisi ya kuwasaidia wananchi badala kuwaghasi, mjadala huu mitandaoni unaonesha kuwa sauti yake ilikuwa ikibeba matamanio yao,” amesema.

Hata hivyo, kuhusu sababu za kutenguliwa kwake, Konga amesema mteuzi ndiye anayetengeneza timu ya viongozi wa kumsaidia kulingana na sifa anazohitaji yeye.

Konga amesema kuondolewa kwa Simbachawene wengi wamesikitika kwa sababu anaonekana alikuwa anaenda na sauti ambayo wananchi wanataka kuisikia.

“Kuhusu uteuzi uliofanyika mwenye mamlaka ndiye anayejua vizuri, ubora na udhaifu wa anaowateua na kuwatengua. Kwa Simbachawene kutenguliwa kwake hatuwezi kujua huenda kuna madhaifu ameyaonyesha au kuna nafasi nyingine anataka kupewa,” amesema.

Mtazamo huo umeungwa mkono na Wakili Aloyce Komba, ambaye amesema kuondolewa kwa Simbachawene kwenye Baraza la Mawaziri anaona ni pengo kwa Serikali, akimtaja waziri huyo kuwa alikuwa akionyesha namna wasaidizi wa Rais wanavyopaswa kufanya kazi.

“Kumuondoa Simbachawene mimi ninaona wanaoonyesha nia ya kumsaidia Rais vizuri ndio anaowaondoa, hii inaonyesha pengo la kikatiba inayompa nafasi Rais kufanya uamuzi yake kadiri inavyompendeza bila kubanwa na mamlaka au sheria yoyote,” amesema na kuongeza:

“Huyu Simbachawene hata sijui kwa nini ameondolewa na licha ya ubora wake kwenye nafasi anazoteuliwa amekuwa akipigwa danadana kwa muda mrefu, hawezi kukaa kwenye Baraza la Mawaziri kwa muda mrefu, hata hivyo bado ninaona hili Baraza la Mawaziri ni la muda tutaendelea kuona mabadiliko mengi,” amesema.

Mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa na mwanahabari mkongwe, Jesse Kwayu amesema: “Mabadiliko ya viongozi kwa muda wa chini ya miezi miwili tangu kuwateua yanaacha maswali kwa kuwa taarifa ya Serikali haikusema sababu hizo, hata hivyo ukiangalia uteuzi huu kuwaengua baadhi huku baadhi wakipanda kutoka ndani ya baraza ndani ya muda huu mfupi, inaashiria kuwepo shida ndani ya Serikali.”

Katika mabadiliko hayo yaliyofanywa na Rais Samia, Profesa Kabudi amehamishwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), wizara ambayo haikuwepo wakati Rais anaunda baraza hilo, Novemba 17, 2025.

Profesa Kabudi anakuwa miongoni mwa mawaziri waliotumikia katika wizara hiyo ambayo imekuwa ikiundwa na kuondolewa, kwa kadiri inavyompendeza Rais aliye madarakani na kwa malengo yake mahsusi.

Katika awamu ya kwanza ya Rais Samia, wizara hiyo ilikuwepo na ilikuwa ikiongozwa na George Mkuchika hadi alipostaafu, mwaka jana.

Vilevile, ofisi hiyo ilikuwapo wakati wa Serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambapo waziri wake alikuwa ni Profesa Mark Mwandosya.

Akizungumzia kuteuliwa kwake katika wizara hiyo, Balozi Dk James Nsekela amesema ni suala lililo chini ya mamlaka ya Rais na majukumu ya wizara hiyo ndiye anayeyaamua.

“Uundaji wa wizara na teuzi ni suala analolifanya anayeteua kutokana na mtazamo wake na hafungwi na sheria yoyote kuhusu nani amteue na nani amtengue. Kujadili kuwa wizara hii itafanyaje kazi na nani ameteuliwa au kutenguliwa, haina maana kwani anayewateua ndiye anayejua.

“Kuhusu uteuzi wa Profesa Kabudi kuteuliwa katika Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalumu), nadhani Rais ndiye anayejua hizo kazi maalumu anazotaka kusaidiwa ni zipi, ndiye anayejua anahitaji kusaidiwa nini, hivyo anaamua amteue nani katika nafasi gani,” amesema.

Kwa upande wake, Wakili Peter Madeleka amesema Rais Samia ametumia mamlaka yake ya kikatiba kuunda Wizara hiyo na kumteua Profesa Kabudi huku akisema sifa zake kitaaluma na uzoefu ndizo zimemfanya Rais aone kuwa atafaa kwa majukumu yaliyopo katika wizara hiyo mpya.

“Rais ana mamlaka kikatiba kuteua mawaziri, kuwatengua na kuunda wizara kwa muundo anaoona yeye. Kumteua Kabudi kuwa Waziri wa Ikulu kazi maalumu lipo ndani ya mamlaka ya Rais kwa mujibu wa sheria.

“Ukiniuliza kuhusu Kabudi nitakwambia ni msomi mwalimu mzuri wa chuo ingawa si lazima kuwa msomi ndiyo kuwa kiongozi bora. Kuhusu kuteuliwa kwake nadhani kwa taaluma yake na uzoefu wake Rais amemuona anafaa kupewa jukumu hilo,” amesema.

Kuhusu majukumu maalumu, Madeleka amesema anayajua aliyemteua kwa sababu Ofisi ya Rais ina mambo mengi ya kufanya akisema inaweza kuwa kumtuma kusimamia au kufuatilia mambo mbalimbali yaliyo chini ya Ofisi ya Rais au mengine yoyote anayoona Rais.

Makonda na Wizara ya Habari

Katika hatua nyingine, Rais Samia amempandisha cheo Makonda kutoka kuwa Naibu Waziri na kuwa Waziri katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiwa ni saa chache tangu aliporejea kutoka Morocco kwenye michuano ya AFCON 2025.

Akizungumzia uteuzi wa Makonda na Katambi, mchambuzi wa siasa nchini, Hamduny Marcel amesema ni uteuzi uliozingatia weledi wao akiwataja kuwa vijana shupavu ambao wameaminika kwa uhodari wao wa kazi.

“Makonda ni mwanasiasa mwenye juhudi na anayejifunza haraka, si mtu mwenye kukaa pembeni na kulialia, ni mwanasiasa ambaye amejipambanua kuwa mchapakazi katika kila nafasi alizopitia tangu akiwa Mkuu wa Wilaya Kinondoni, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na uongozi ndani ya chama na baadaye Naibu Waziri,” amesema.

Kuhusu Katambi, amesema amekuwa kijana anayeaminiwa akipewa unaibu waziri katika wizara mbalimbali, kikubwa kilichombeba kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ni taaluma yake ya sheria kwani ana elimu.