Venezuela yawaachia huru waandishi, wanaharakati, wapinzani

Venezuela. Serikali ya Venezuela imewaachia huru watu kadhaa waliokuwa kizuizini wakiwamo vigogo wa upinzani, wanaharakati na waandishi wa habari sambamba na raia wa ndani na wa kigeni, katika kile ilichokieleza ni hatua ya kutafuta amani.

Hata hivyo, hatua hiyo imekuja ikiwa ni wiki moja imepita tangu aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro akamatwe na majeshi ya Marekani ili kufikishwa mbele ya sheria kwa tuhuma za biashara haramu ya dawa za kulevya.

Rais wa Marekani, Donald Trump ambaye amekuwa akiwashinikiza washirika wa Maduro wanaoongoza nchi kwa sasa, wakubaliane na dira yake kuhusu mustakabali wa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Rais Trump amesema hata kuachiwa kwa wafungwa hao, kumekuja baada ya Marekani kupeleka ombi hilo.

Katika mahojiano na Fox News jana usiku, Rais Trump aliisifu serikali ya Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez akisema: “wamekuwa wazuri sana. … Kila tulichokitaka, wametupa.”

Jorge Rodriguez, ndugu wa Rais wa mpito na Mwenyekiti wa Bunge la Taifa la Venezuela, amesema idadi kubwa ya watu ingeachiwa huru, lakini hadi usiku wa manane wa Alhamisi haikuwa wazi ni akina nani wala ni watu wangapi wanaoweza kuachiwa huru.

Kwa muda mrefu, serikali ya Marekani na upinzani ya Venezuela, wanasema wameridhishwa na hatua ya kuachiliwa kwa wingi kwa wanasiasa, wakosoaji na wanajamii waliokamatwa.

Hata hivyo, Serikali ya Venezuela kwa upande wake, imeendelea kusisitiza kuwa haina wafungwa wa kisiasa.

“Chukulieni hili kama ishara ya serikali ya Bolivaria ya Venezuela, inayolenga kwa mapana kutafuta amani,” imesema serikali hiyo.

Kuachiwa kwa watu mashuhuri

Miongoni mwa walioachiwa huru ni Biagio Pilieri, kiongozi wa upinzani aliyekuwa sehemu ya kampeni ya urais ya 2024 na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Maria Corina Machado.

Hiyo ni kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za wafungwa la Foro Penal, lenye makao yake makuu katika mji wa Caracas.

Kiongozi mwingine aliyeachiwa huru ni Enrique Marquez, aliyewahi kuwa kiongozi wa chombo cha usimamizi wa uchaguzi na mgombea katika uchaguzi wa urais wa 2024.

Video zilizosambazwa na waandishi wa habari kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha Marquez na Pilieri wakikumbatiana na wapendwa wao mitaani nje ya gereza.

Video moja inamuonyesha Márquez akiwa na tabasamu akifanya mawasiliano ya video na wanafamilia wake, akisema, “Hivi karibuni nitakuwa nanyi nyote.”

Raia watano wa Hispania akiwamo wakili mashuhuri na mtetezi wa haki za binadamu Rocío San Miguel nchini humo, aliachiwa huru alasiri, na kadri usiku ulivyoendelea taarifa ziliendelea kutoka za wafungwa wengine kuachiwa.

Nje ya gereza moja lililopo mjini Guatire, mashariki mwa Caracas, ndugu na jamaa waliokuwa wakisubiri kwa saa nyingi, walisikika wakipiga kelele wakisema ‘Uhuru! Uhuru!’

Serikali ya Venezuela ina historia ya kuwaachia huru watu waliokamatwa kwa sababu za kisiasa, hatua ambayo mara nyingi hutafsiriwa kama ishara ya utayari wa kuanzisha au kuendeleza mazungumzo.

Hivyo, kuachiliwa kwa watu hao kulikofanyika jana Alhamisi Jnauri 8, 2026, ni tukio la kwanza la aina hiyo tangu Nicolás Maduro aondolewe madarakani.

Makundi ya kutetea haki za binadamu pamoja na wanachama wa upinzani wamepokea hatua hiyo kwa tahadhari na matumaini, ingawa bado haijawa wazi inaashiria nini hasa.

Baadhi wanaiona kama dalili za awali za mwelekeo wa serikali ya mpito, huku wengine wakitafsiri kama ishara ya kisiasa inayolenga kuiridhisha serikali ya Rais wa Marekani, ambayo imewaruhusu waaminifu wa Maduro kuendelea kubaki madarakani huku ikiendeleza shinikizo kupitia vikwazo vikali vya kiuchumi.