Wananchi washauriwa kufanya uchunguzi wa afya zao

Arusha. Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi ametoa wito kwa wananchi kuwa na tabia ya kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kujua hali zao kwasababu takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa vifo milioni 17 ambavyo ni sawa na asilimia 32 duniani vinasababishwa na magonjwa ya moyo.

Amesema hayo leo Ijumaa, Januari 9, 2026 wakati akifunga kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya bure kwa wananchi zaidi ya 3,000 yaliyokua yakitolewa na madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya Arusha Lutheran Mediacal Center (ALMC) jijini Arusha.

“Takwimu za hapa nchini  zinaonyesha mkoa wa Arusha una watu wengi wenye matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwemo magonjwa yasiyoambukiza ikihusisha magonjwa ya Moyo. Magonjwa haya yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, kisukari, na saratani, ni mojawapo ya changamoto kubwa za afya duniani,”amesema Dk Samizi.

Ameongeza kuwa takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa magonjwa hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa vifo na mzigo wa kiafya katika jamii nyingi na kutoa wito kwa wananchi kujiunga na mpango wa bima ya afya kwa wote ili waweze kupata huduma za matibabu kwa urahisi na ni nguzo muhimu katika kufanikisha lengo la afya kwa wote.

“Wote tunatambua hali zetu zilivyo hivyo kujiunga na bima ya afya kunalinda familia dhidi ya mshtuko wa kifedha unaoweza kujitokeza pindi mmoja wetu anapokumbwa na ugonjwa unaohitaji matibabu ya muda mrefu au ya kibingwa, ninatoa wito kwa jamii kuchukua hatua mapema kwa kujiunga na mifumo ya bima ya afya utakao anza kufanya kazi hivi karibuni,”amesema Dk Samizi.

Dk Samizi amesema utendaji kazi wa pamoja  taasisi mbili za JKCI na ALMC ni muunganiko  muhimu ikizingatiwa mkoa wa Arusha ni sehemu ya kuandaa mashindano makubwa ya AFCON mwaka 2027 na ajenda nzima ya masuala ya Tiba Utalii hivyo amerishishwa na maboresho yanayoendelea.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema wameanza kufanya maboresho makubwa kwenye vitengo vya wagonjwa mahututi (ICU), maabara na kusimikwa vifaa vya kisasa vinavyotumia Akili Unde na kufunga mifumo ya kuwafatilia wagonjwa walioruhusiwa kupitia mifumo hiyo.

“Tunataka hospitali hii iwe ya mfano katika ukanda huu wa Afrika Mashariki,tutaimarisha huduma kwa kuwafata wananchi walipo tunaweka mikakati ya kufanya kambi mbalimbali wilayani ili kuwawezesha wananchi kupata huduma huko walipo,”amesema Dk Kisenge.

Kwa upande wake,Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Godson Mollel ameishukuru serikali kwa kuingia ubia kwaajili ya kutoa huduma kwa karibu na zenye ufanisi kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Amesema ushirikiano kati ya serikali na taasisi za dini unapaswa kuendelezwa kwa maslahi mapana ya kuwahudumia wananchi ambao wanazitegemea taasisi hizo ziwahudumie wakati wote.