Wasiorejesha mikopo ya asilimia 10 kukamatwa

Maswa. Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney ameagiza kukamatwa na kufikishwa mahakamani watu wote waliokopa mikopo ya serikali ya asilimia 10 kupitia makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambao wameshindwa kurejesha fedha hizo kwa wakati.

Ametoa agizo hilo leo Ijumaa Januari 9,2025 wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya hiyo baada ya kusomwa taarifa ya halmashauri ya wilaya ya Maswa kuwa inadai jumla ya Sh752 milioni kutoka kwa wanufaika waliopatiwa mikopo hiyo.

Amesema lengo la serikali kutoa mikopo hiyo ni kuinua wananchi kiuchumi, hivyo fedha hizo lazima zirejeshwe ili ziwanufaishe wananchi wengine wanaohitaji mikopo kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza shughuli za kiuchumi.

“Fedha hizi si sadaka, ni fedha za serikali zinazotokana na kodi za wananchi. Ni wajibu wa aliyekopa kurejesha kwa wakati ili na wengine wapate fursa ya kukopa, tunataka fedha hizi ziwe kwenye mzunguko hivyo jeshi la Polisi pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mhakikishe watu hao wanarejesha fedha za serikali,” amesema.

Anney ameeleza kuwa baadhi ya wakopaji wamekuwa wakikwepa urejeshaji licha ya shughuli zao kuendelea, hali inayokwamisha lengo la serikali la kuwezesha maendeleo ya makundi maalum.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Julius Ikongora amesema halmashauri imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa notisi, kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutoa elimu, lakini bado baadhi ya wanufaika wamekaidi masharti ya mikopo.

“Hatuna nia ya kumuonea mtu, lakini sheria lazima ifuate mkondo wake. Tutachukua hatua za kisheria kwa wale wote wanaokaidi urejeshaji,” amesema.

Amesisitiza kuwa halmashauri itaendelea kutoa elimu, lakini kwa wale wote wanaokaidi kwa makusudi, hatua za kisheria zitachukuliwa bila kusita.

Jane Richard ni mkazi wa mjini Maswa amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kurejesha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.

“Wapo watu wamekopa na biashara zao zinaendelea vizuri lakini hawarudishi fedha. Serikali ikikaa kimya wengine watakata tamaa ya kulipa,” amesema.

Naye Mashaka Husein mkazi wa Lalago wilayani humo amesema mikopo hiyo imesaidia wengi lakini inahitaji uwajibikaji.

“Mikopo hii imetusaidia sana, lakini ukikopa lazima urudishe. Bila hivyo, haki kwa wengine haitakuwepo,” amesema.

Mary Samson ni mkazi wa Malampaka amesema kuwa ni vizuri serikali ikatoa muda au kufanya tathmini kwa wakopaji waliokumbwa na changamoto za kibiashara.

“Kuna waliokumbwa na hasara au magonjwa ni vyema serikali ikaangalia kesi kwa kesi,” amesema .