KOCHA Mkuu wa Bunda Queens, Alley Ibrahim amesema ili kukiongezea nguvu kikosi chao kwenye Ligi Kuu ya Wanawake, watawapandisha wachezaji wao watano kutoka kwenye kituo chao cha kukuza vipaji vya soka (Bunda Queens Program).
Timu hiyo Desemba 13, 2025 ilikumbana na adhabu ya kupokonywa pointi tano, kutozwa faini ya Sh5 milioni na mwenyekiti wake kufungiwa mwaka mmoja, baada ya kushindwa kufika kwenye mchezo dhidi ya JKT Queens, jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo ulipaswa kuchezwa Desemba 8, mwaka jana kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamhuyo, hivyo, JKT Queens ilipewa alama tatu na ushindi wa mabao 3-0.
Hata hivyo, tayari imeshazilipa alama hizo na imeanza kujipata kwa kuona mwanga baada ya juzi kupata ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Bilo FC kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibrahim amesema sehemu kubwa ya wachezaji watakaopandishwa wamekuwa wakifundishwa pamoja na kikosi cha kwanza, hivyo hakutakuwa na changamoto yoyote katika kuisaidia timu hiyo.
“Mimi kama mkuu wa benchi la ufundi niseme tu tutaongeza wachezaji lakini kutoka kwenye timu yetu ya pili ya Bunda Queens Program, tuna programu pale kwenye timu yetu tunapandisha wachezaji,” amesema Ibrahim na kuongeza;
“Tutawapandisha hao wachezaji karibia watano ambao wataenda kuongeza nguvu kwa dada zao. Tunapandisha mabeki na mshambuliaji mmoja ili kuongeza nguvu pale mbele.”
Akizungumzia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Bilo FC, amesema changamoto walizopita mwanzo zimewaimarisha kwani hawakutaka kukata tama, walipambana wakiwa na lengo la kupata ushindi na kuendelea kusimama kwenye malengo yao.
Amesema ukiwa ni msimu wao wa tatu kwenye Ligi Kuu wamepata uzoefu, kadri wanavyoendelea kucheza ndiyo wanapata kitu kipya kwa wachezaji na benchi la ufundi.
“Tumeanza msimu kwa changamoto ngumu tumenyang’anywa pointi kutokana na matatizo ya nje ya uwanja, lakini tulikaa tukatulia tukawaambia watoto wafanye kazi, sasa tumerudi naamini tutaendelea kuvuna pointi.”
