Watoto wawili wa familia moja walivyokufa maji

Arusha. Vilio na majonzi vimetanda katika familia ya Joachim Laizer, iliyopoteza watoto wawili kwa wakati mmoja, ambao wamekufa wakiogelea.

Abednego (13) na Ebenezer Joachim (9), walizama kwenye kina kirefu cha maji wakiogelea kwenye bwawa la kuogelea.

Tukio hilo lilitokea Januari 7, 2026, ndani ya Hoteli ya Kilimanjaro Food, eneo la Sakina, jijini Arusha.

Taarifa za awali zinadai watoto hao walipelekwa hotelini hapo na mama yao kwa ajili ya kuogelea.

Inaelezwa mama yao aliwaacha kwa uongozi wa hoteli akaenda kufanya ununuzi wa mahitaji yao ya shule.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, amethibitisha tukio hilo leo Januari 9, 2026 akieleza uchunguzi bado unaendelea na taarifa rasmi kwa umma itatolewa.

“Ni kweli tukio limetokea, lakini uchunguzi bado unaendelea. Taarifa kamili itatolewa pindi uchunguzi utakapokamilika,” amesema.

Akizungumza nyumbani kwake, Joachim Laizer, baba wa watoto hao amesema Abednego alikuwa amemaliza darasa la saba na alikuwa anatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, huku mdogo wake Ebenezer alitarajiwa kuanza darasa la nne.

Amesema anahisi kuna uzembe uliosababisha vifo vya watoto wake, akisisitiza ilipaswa kuwapo uangalizi wa mtu mzima wakati watoto wanapoogelea.

“Nikiwa namhudumia baba yangu Hospitali ya KCMC Moshi, nilipigiwa simu nikaelezwa kuwa watoto walizidiwa na maji walipokuwa wanaogelea na wamewahishwa Hospitali ya St. Joseph. Nilijiuliza inakuwaje watoto wanaogelea bila msimamizi? Nilishangaa sana,” amesema.

Amesema ingawa watoto wake hawawezi kurejea, anataka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika ili iwe fundisho kwa maeneo mengine ya burudani.

“Natamani mwenye hoteli achukuliwe hatua, si kwa ajili yetu tu bali iwe funzo kwa wengine. Pia hoteli yenyewe ichukue hatua za kuhakikisha usalama wa watoto wengine kwa wakati mwingine,” amesema.

Mwananchi lilifika hotelini hapo, ambako kiongozi ambaye hakujitambulisha jina zaidi ya kueleza ni meneja uendeshaji amesema tukio hilo ni kweli limetokea na hakuna uzembe, bali ni ajali kazini.

“Huo uzembe mnasema ninyi sisi hatuna taarifa za uzembe wowote kama mnataka taarifa zaidi nendeni Polisi wana taarifa zaidi za tukio,” alisema jana Januari 8, 2026.

Hata hivyo, mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo ambaye hakuwa tayari kutajwa jina, akiwanukuu wenzake, anadai wakati watoto hao wakiogelea mmoja alizama majini kwenye kina kirefu ambako watu wazima huogelea, hivyo mwenzake alijaribu kumuokoa, ndipo wote wawili wakazama.

“Kawaida watoto wakienda kuogelea kunakuwa na msimamizi ambaye hufuatilia mienendo yao, wasisogee penye kina kirefu lakini siku hiyo hakukuwa na mtu anayewafuatilia ndiyo maana wakakosa msaada wa haraka hadi mauti yakawakuta,” amedai.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimnyaki, Samweli Meliyo, amesema tukio hilo limewashtua na kuwasikitisha.

“Kupoteza watoto wawili kwa mkupuo ni pigo kubwa kwa familia na jamii, tunaomba vyombo vya ulinzi na usalama vifanye uchunguzi wa kina kubaini kama kulikuwa na uzembe na iwapo utabainika, hatua za kisheria zichukuliwe,” amesema.

Ingawa polisi halijathibitisha, inadaia watu wanne wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano kuhusu tukio hilo wakati uchunguzi ukiendelea.