WATU wanajiuliza itakuwaje mechi ya Yanga dhidi ya Singida Black Stars leo Ijumaa katika nusu fainali ya pili ya Kombe la Mapinduzi 2026 itakayochezwa saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.
Hiyo ni baada ya jana Alhamisi kushuhudia nusu fainali ya kwanza katika Kombe la Mapinduzi 2026 kati ya Azam na Simba. Mshindi wa jana, atacheza fainali na mshindi wa leo itakayopigwa Januari 13, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Si kwa ubaya, bali kinachowafikirisha wengi ni namna vikosi vya Yanga na Singida Black Stars vilivyo kutokana na baadhi ya wachezaji wamehama kwa mkopo kutoka upande mmoja kwenda mwingine, hivyo wanakutana na waajiri wao.
Frank Assinki ametua Yanga tangu dirisha kubwa la usajili akipishana na Nickson Kibabage aliyeenda Singida, lakini yeye hatakuwapo kwa sababu alikuwa Morocco na kikosi cha Taifa Stars.
Pia Mohamed Damaro na Marouf Tchakei wametua Yanga kipindi hiki cha dirisha dogo wakitokea Singida. Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Singida, Hussein Masanza, waneruhusu nyota hao kutumiwa na Yanga dhidi yao, hivyo, kazi ipo leo.
Katika mjadala wa itakuwaje mechi hiyo, juzi walikutana maofisa habari wa timu nne, Ally Kamwe (Yanga), Ahmed Ally (Simba), Hasheem Ibwe (Azam) na Hussein Masanza (Singida Black Stars), katika mazungumzo yao, Ahmed Ally alisikika akimuuliza Ally Kamwe: “Mechi yenu na Singida mnachezaje, au mnaingia uwanjani mnakaa katikati, mnaanza kuchaguana, wewe nenda huku, na wewe nenda huku, ndio mtafanya hivyo?”
Hata hivyo, mechi ya Yanga dhidi ya Singida Black Stars kwa nje inaonekana nyepesi, lakini ndani ya uwanja, kuna vita kubwa ya wachezaji wanaopambana kusaka matokeo mazuri.
Kitendo cha Yanga kumchukua kwa mkopo Mohamed Damaro kutoka Singida, imetajwa kuwa ni usajili mzuri uliofanywa na Wanajangwani hao baada ya siku za hivi karibuni kuikosa huduma ya Mudathir Yahya aliyeumia, huku pia mzigo mkubwa ulikuwa kwa Duke Abuya ambaye katika Kombe la Mapinduzi, amepewa kitambaa cha unahodha.
Damaro baada ya mechi ya kwanza dhidi ya KVZ kutokea benchini na kucheza kwa dakika 29 akichukua nafasi ya Abuya, iliyofuatia dhidi ya TRA United walizima pamoja viungo hao ambapo Abuya alicheza juu, Damaro chini.
Katika mechi ya leo, hapo kati kutakuwa na vita kubwa sana ambapo upande wa Singida kuna Morice Chukwu ambaye anashikilia rekodi ya kuwa nyota pekee mwenye tuzo mbili za mchezaji bora wa mechi katika Kombe la Mapinduzi ‘26.
Chukwu katika eneo hilo, mara kwa mara amekuwa akicheza sambamba na Ibrahim Imoro ambaye kiuhalisia ni beki wa kushoto lakini kocha David Ouma amelazimika kumpanga kiungo wa kati kutokana na kuwakosa Khalid Aucho (Uganda) na Khalid Habib ‘Gego’ (Tanzania) waliokuwa na majukumu ya kushiriki AFCON 2025 nchini Morocco.
Safu zote kila upande zitakuwa bize muda wote wa mechi kutokana na kuwepo kwa wachezaji hatari katika timu hizo wanaocheza maeneo hayo.
Kwa Singida, Elvis Rupia na Joseph Guede ambaye aliwahi kuichezea Yanga kabla ya kuhamia Singida, wanaongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Guede na Rupia wamekuwa wakicheza pacha, huku Idriss Diomande akiongeza nguvu eneo la ushambuliaji hali iliyofanya Singida kumaliza hatua ya makundi ikiwa na mabao matano yaliyofungwa na Guede na Diomande kila mmoja mawili, huku Emmanuel Keyekeh akitupia moja.
Timu hiyo pia inahitaji kurekebisha safu ya ulinzi kutokana na kushindwa kujizuia ikiruhusu bao kila mechi, hali hiyo inadhihirisha kwamba, inapokutana na timu yenye uwezo wa kufunga mabao, itakuwa hatarini.
Yanga imekuwa imara katika kujilinda na kushambulia. Katika mechi mbili ilizocheza, imefunga mabao manne ikiwa na wastani wa kufunga mabao mawili kila mechi, huku nyavu zake zikiwa bado hazijaguswa.
Celestine Ecua, Pacome Zouzoua na Emmanuel Mwanengo, wamekuwa tegemeo eneo la ushambuliaji, huku ulinzi ukiongozwa na Assinki, Aziz Andabwile na kipa Aboutwalib Mshery.
Katika ulinzi, Yanga imepata nguvu baada ya Yao Kouassi kurejea akifanikiwa kucheza mechi iliyopita dhidi ya TRA United.
YANGA WAKONGWE, SINGIDA WAGENI
Hii ni mara ya kwanza Singida Black Stars inashiriki Kombe la Mapinduzi. Kumbuka timu hii ilikuwa ikifahamika kwa jina la Ihefu kabla ya kuuzwa na kuhamisha makazi kutoka Mbarali mkoani Mbeya hadi Singida.
Mara ya mwisho timu kutoka Singida kushiriki mashindano haya ilikuwa Singida Big Stars ambayo baadaye ikabadilishwa jina na sasa inaitwa Fountain Gate, imeweka ngome yake pale Manyara ikitumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa kwa mechi zake za nyumbani.
Sasa basi, ugeni wa Singida Black Stars katika Kombe la Mapinduzi si kitu, kwani imeonyesha ushindani mkubwa hadi kutinga nusu fainali.
Ikiwa kundi A, Singida Black Stars ilimaliza nafasi ya pili kwa pointi tano, ikishinda mechi moja dhidi ya Mlandege (3-1), kisha sare mbili dhidi ya Azam (1-1) na URA (1-1).
Singida Black Stars ilikuwa ya kwanza kufuzu nusu fainali, hivyo unaona si timu ya kubeza ukizingatia kwamba Septemba mwaka jana ilibeba Kombe la Kagame, mashindano yaliyofanyika jijini Dar es Salaam huku timu hiyo ikishiriki kwa mara ya kwanza.
Hivi karibuni timu hiyo imefanya mabadiliko ya benchi la ufundi kwa kumbadilishia majukumu aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Miguel Gamondi kuwa mkurugenzi wa ufundi, huku David Ouma aliyekuwa kocha msaidizi sasa akitambulika kama kocha mkuu, huku ikimuajiri Othmen Najjar kuwa meneja mkuu.
Licha ya kwamba ni mara ya kwanza zinakwenda kukutana katika Kombe la Mapinduzi, Yanga na Singida Black Stars zinafahamiana.
Mara ya mwisho timu hizo zimekutana Juni 29, 2025 katika fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) iliyochezwa Uwanja wa New Amaan, hivyo mechi ya Ijumaa hii itakumbushia miezi sita iliyopita.
Ukongwe wa Yanga katika Kombe la Mapinduzi unatokana na mwaka 2007 michuano hii ilipoanza kushirikisha timu mchanganyiko kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Yanga ilikuwa bingwa wa kwanza. Ushiriki wao wa mara kwa mara ukawapa taji jingine mwaka 2021 na sasa inalisaka kwa mara ya tatu.
Kocha Pedro Goncalves anafanya juhudi kubwa kuhakikisha anafuzu fainali na kwenda kubeba kombe la kwanza tangu atue Yanga.
Pedro amechukua nafasi ya Romain Folz aliyeshinda Ngao ya Jamii kwa kuichapa Simba bao 1-0.
Timu hizi zinashuka dimbani leo zikiwaza kutinga fainali na kwenda kushinda ubingwa ili kuondoka na kibunda cha Sh150 milioni ambacho hukabidhiwa bingwa. Imepanda kutoka Sh100 milioni.
Lakini kwa kuingia tu fainali, uhakika wa kupata Sh100 milioni upo kwani ndicho kiasi anachopewa atakayemaliza nafasi ya pili katika michuano hiyo ya mwaka huu, ikiwa imepanda kutoka Sh70 milioni.
