Dk Mwinyi: Miundombinu ya elimu inakidhi matakwa karne ya 21

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema wanajivunia miundombinu ya elimu inayojengwa Zanzibar kwenda sambamba na matakwa ya karne ya sasa ya sayansi na teknolojia.

Hivyo, amesema serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia hatua itakayowawezesha wanafunzi kuongeza ufanisi na kufanya vizuri zaidi katika masomo yao.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Januari 10, 2026, katika ufunguzi wa shule ya mfano ya Sekondari ya Ramadhan Haji Faki Gamba, Wilaya ya Kaskazini A Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema uwepo wa miundombinu bora ikiwemo maabara za kisasa, vyumba vya Tehama pamoja na maktaba zenye vitabu vya kutosha, ni nyenzo muhimu zitakazowasaidia wanafunzi kuimarisha uelewa wao na kufanya vizuri katika mitihani ya taifa.

Rais Mwinyi amebainisha kuwa katika shule hiyo kuna jengo la mgahawa kwa ajili ya wanafunzi kupata chakula, jengo la walimu na dahalia ya wanafunzi

“Hivi sasa tutaondokana na shule za kawaida za mabanda na badala yake, kuwa na shule zenye mabweni, migahawa na nyumba za walimu,” amesema.

Rais Huyo amesema mara nyingi wanafunzi wanapata changamoto ya kukaa nje ya shule, hali inayowafanya wasiweze kufanya vizuri kwa sababu imethibitika wakikaa katika bweni maendeleo yao ya masomo yanakua.

“Hatuna shaka katika shule hii vijana wetu watapata mazingira mazuri ya kujifunzia na kuishi ili waweze kufanya vizuri zaidi katika mitihani ya taifa,” amesema.

Amesisitiza serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu kwa kuzingatia mahitaji ya walimu, vifaa vya kufundishia pamoja na teknolojia, ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu yenye ubora na inayowaandaa kukabiliana na soko la ajira.

Akizungumzia fidia za wananchi waliokuwa wakilima eneo hilo, amesema watapatiwa huku akisema amepokea ombi la wazee wa kijiji hicho kutaka kujengewa nyumba za maendeleo.

Ameipongeza wizara kwa kazi nzuri ya kusimamia ujenzi wa shule mbalimbali za msingi na sekondari kwa maeneo ya Unguja na Pemba na mkandarasi Zeccon Company Limited, iliyojenga shule hiyo na mshauri elekezi, Arqes Afrika.

Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khadija Salum Ali amesema katika eneo hilo bado wananchi wanadai fidia na mchakato wa malipo unaendelea.

Amesema wizara itahakikisha kila mwenye haki yake anaipata kupitia kamati iliyoundwa kupitia tathmini ya fidia.

Waziri Ali amemuomba Rais Mwinyi kuridhia shule hiyo kuipa jina la Ramadhan Haji Faki, aliyekuwa miongoni mwa walioshiriki Mapinduzi ili kumuenzi.

Amesema marehemu Ramadhan alikuwa mjumbe wa watu 14 wa kamati ya Mapinduzi Zanzibar ya mwaka 1964 na aliwahi kutumikia serikali kwa nyadhifa mbalimbali ikiwemo waziri kiongozi kwa vipindi viwili.

Akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdulla Said amesema mradi wa shule hiyo umejengwa chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kushirikiana na serikali ambao unahusisha shule, nyumba za walimu, bweni na eneo la chakula.

Katibu Khamis amesema ujenzi wa shule hiyo ulianza Machi mwaka jana na sasa ujenzi umefikia asilimia 97 unaogharimu Sh11.02 bilioni na kati ya hizo, mkandarasi ameshalipwa Sh8.8 bilioni.