Habari njema kwa waliofeli mtihani kidato cha pili 2025

Dar es Salaam. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloya imetoa ahueni kwa wanafunzi waliofeli katika mitihani yao ya kidato cha pili na sasa badala ya kukariri darasa, watafanyiwa programu maalumu huku wakiendelea na kidato cha tatu.

Ahueni hiyo imetangazwa leo Jumamosi Januari 10, 2026 na Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa katika taarifa yake aliyoitoa kwa umma.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni saa chache zimepita tangu Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya kidato cha pili ambapo jumla ya wanafunzi wa shule 705,091, sawa na asilimia 86.93, wamefaulu kuendelea na kidato cha tatu kwa kupata daraja la kwanza hadi la nne ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.52 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2024.

Hata hivyo, mwaka 2025, kwa mara ya kwanza, mtihani wa kidato cha pili ulifanyika katika mikondo miwili ukihusisha mkondo wa amali ambapo matokeo yanaonyesha wanafunzi wamefaulu kwa asilimia 100 katika masomo ya fani za amali za uhandisi, umeme, mitambo, magari na Tehama.

Katika masomo ya fani za amali zisizo za uhandisi, ikiwemo kilimo na chakula, ukarimu na utalii, mavazi na ushonaji, michezo na sanaa za ubunifu, masomo manane kati ya 14 wanafunzi wamefaulu kwa asilimia 100.

Hata hivyo, matokeo ni mabaya kwa somo la Leather Goods and Footwear ambapo ni wanafunzi watatu pekee kati ya 20, sawa na asilimia 15, ndiyo wamefaulu.

Katika taarifa yake hiyo, Kamishna wa Elimu amesema: “Ninaelekeza kwamba wanafunzi ambao hawakufikia alama za ufaulu za kidato cha pili, mwaka 2025 waendelee na kidato cha tatu mwaka 2026 badala ya kukariri (kurudia) kidato cha pili.

“Wanafunzi hao watapewa programu maalumu rekebishi (remedial programme) itakayotolewa wakati wakiendelea na masomo yao ya kidato cha tatu,” amesema Dk Mtahabwa.

Kamishna huyo ameeleza kuwa uamuzi huo unazingatia kwamba mitaala iliyoboreshwa inatekelezwa kwa awamu na wanafunzi waliofanya upimaji wa kidato cha pili mwaka 2025 walitumia mtaala wa zamani na watamaliza kidato cha nne kwa kutumia mtala huo wa zamani.

“Wanafunzi wanaoingia kidato cha pili mwaka 2026 watatumia mtaala ulioboreshwa ambao walianza kuutumia kidato cha kwanza, hivyo endapo wanafunzi walioshindwa kufikia alama za ufaulu watarudia kidato cha pili mwaka 2026, watalazimika kutumia mtaala ulioboreshwa ambao hawakuanza nao kidato cha kwanza. Hii italeta changamoto kubwa katika ujifunzaji na ufundishaji,” amefafanua zaidi Kamishna huyo.

Hata hivyo, amesema maelekezo hayo yanawahusu wanafunzi wa kidato cha pili kwa mwaka 2025 waliopimwa kwa kutumia mtaala wa zamani na kwa wanafunzi wa mkondo wa elimu ya amali walioshindwa kufikia alama za ufaulu wataendelea na utaratibu wa kukariri (kurudia) kidato cha pili katika mwaka 2026.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa hii ni kwa sababu wao walianza kutumia mtaala ulioboreshwa tangu kidato cha kwanza.

“Ni matarajio yetu kuwa wakuu wa shule zenye wanafunzi husika watatekeleza maelekezo haya kwa ukamilifu na kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanafundishwa na kujifunza ipasavyo ili kupata umahiri uliokusudiwa,” inasema taarifa hiyo.