KITUO CHA UMEME KIKULETWA KUWA KITOVU CHA MAFUNZO JADIDIFU AFRIKA

Na Seif Mangwangi, Hai

SERIKALI imesema imewekeza kwenye ujenzi wa mradi wa EASTRIP ili kukifanya Chuo cha Ufundi Arusha, kupitia Kituo cha Umahiri Kikuletwa, kuwa kitovu cha mafunzo ya nishati jadidifu (renewable energy) kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Afrika.

Hayo yameelezwa leo 6 Januari 2026 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa EASTRIP Kikuletwa ulioko Wilaya ya Hai Kilimanjaro.

Wanu amesema kituo hicho cha umahiri cha Kikuletwa ni cha kimkakati kwa sababu kitatoa mafunzo ya vitendo katika uzalishaji wa nishati jadidifu (nishati ya nguvu ya maji, nishati ya nguvu ya jua, nishati nguvu ya upepo, na nishati ya bioanuwai.

“ Aidha kituo hiki kitaandaa na kuwapa ujuzi (skills) vijana watakaofanya kazi katika miradi mikubwa ya kitaifa na kimataifa kama vile Bwawa la Uzalishaji Umeme la Mwalimu Nyerere na kitachochea ushirikiano wa kikanda kwa kupokea wanafunzi na wataalamu kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya mafunzo na tafiti,” amesema.

Ameupongeza uongozi wa chuo cha ufundi Arusha kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi hususani wanawake, “ haya ni mafanikio makubwa sana Kwa nchi yetu, katika kumuinua mtoto wa kike,” amesema

Amesema katika utekelezaji wa Sera ya Elimu 2014 toleo la 2023, Serikali itaendelea kuboresha Chuo cha Ufundi Arusha ili vijana waliochagua mkondo wa amali wapate fursa za kujiunga na Chuo hiki kinachosifika kwa ubora.

Wanu amesema hatua ya Wizara ya Nishati kuunganisha Chuo cha Ufundi Arusha na taasisi ya International Solar Alliance ambayo imeingia makubaliano ya kuanzisha Kituo Maalum cha Rasilimali ya Nishati ya jua ni ya kupongezwa.

“Kituo hiki kitatoa huduma kwa pamoja (one stop Center) kwa ajili ya kujenga uwezo, upimaji (testing), uwekwaji wa viwango (standardization) na uendelezaji wa teknolojia za nishati ya jua. Uwepo wa kituo hiki utachochea maendeleo kwenye uvumbuzi wa vifaa vinavyotumia nishati ya jua hapa nchini,” amesema.

Akitoa taarifa ya chuo cha ufundi Arusha, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Chacha Musa amesema uwepo wa Kituo cha Umahiri cha Kikanda cha Mafunzo ya Nishati Jadidifu chini ya chuo hicho kutafungua fursa nyingi kwa Chuo, kwa jamii ya Kikuletwa na Taifa.

Amesema chuo kimejipanga kuhamasisha wanafunzi wa kitanzania wanaosoma mkondo wa amali wachague kubobea katika mafunzo ya nishati jadidifu yanayotolewa chuoni hapo katika Kampasi ya Kikuletwa ili kuchangia kuzalisha wataalamu wengi zaidi ambao watashiriki katika utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa matumizi ya nishati safi.

“Tutahakikisha kuwa tunatangaza uwepo wa kituo hiki cha umahiri kwa makampuni yanayohusika na uzalishaji wa umeme katika nchi mbalimbali ili watumie kituo hiki kwa ajili ya kuwapatia mafunzo wafanyakazi wao,” amesema.

Amesema hatua hiyo itaiingizia Tanzania fedha za kigeni na kuboresha utoaji wa mafunzo na utajitangaza zaidi kimataifa ili kuwavutia wanafunzi kutoka nchi mbalimbali kuja kupata mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi Kikuletwa.

Profesa Chacha amesema mafunzo yatakayotolewa yatakuwa ya ubora wa hali ya juu kwa kuwa Chuo cha Ufundi Arusha ni miongoni mwa vyuo vichache sana duniani vinavyomiliki mtambo wa kufua umeme kwa nguvu za maji.

“Hatua hii pia italiingizia taifa letu fedha za kigeni, tutaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi na viwanda mbalimbali katika utoaji mafunzo yanayoendana na mahitaji ya soko,” amesema.

Ameishukuru Wizara ya Nishati kwa kuwaunganisha na taasisi ya International Solar Alliance (ISA) ili kuanzisha Kituo Maalum cha Rasilimali za Nishati ya jua.

“ Kituo hiki kitatoa huduma kwa pamoja (one stop Center) kwa ajili ya kujenga uwezo, upimaji (testing), uwekwaji wa viwango (standardization) na uendelezaji wa teknolojia za nishati ya jua. Uwepo wa kituo hiki utachochea maendeleo kwenye uvumbuzi wa vifaa vinavyotumia nishati ya jua,” amesema.

Aidha Profesa Chacha amesema chuo hicho kimepata mafanikio makubwa ikiwemo kufanikiwa kutengeza mitaala mipya ishirini na saba (27) inayokidhi mahitaji ya viwanda katika programu zinazohusiana na nishati jadidifu.

“ Kati ya hizo jumla ya mitaala kumi na mbili (12) imetengenezwa kwa programu za muda mrefu na mitaala kumi na tano (15) katika programu za muda mfupi,” amesema.

Pia amesema jumla ya wakufunzi thelathini na moja (31) wamefanikiwa kupata mafunzo ya viwandani kwa muda wa kuanzia mwezi mmoja na kuendelea ili kuweza kuendana na mabadiliko ya teknolojia na ujuzi unaohitajika katika viwanda.

“ Jumla ya watumishi kumi na tatu (13) wamefanikiwa kupata nafasi za kujifunza katika taasisi mbalimbali za nje ya nchi, Jumla ya makubaliano (memorundum of understanding) kumi na sita (16) na viwanda na taasisi nyingine za kielimu za nje ya nchi imefikiwa,” amesema.

Amesema chuo kimefanikiwa kufanya ufuatiliaji wa wahitimu kila mwaka ambapo katika wahitimu wa mwaka 2024 asilimia 72.5% walifanikiwa kupata ajira katika muda wa miezi sita baada ya kuhitimu na kwa upande wa wahitimu wa kike asilimia 62.6% walifanikiwa kupata ajira katika muda wa miezi sita baada ya kuhitimu.

Mafanikio mengine ni pamoja na chuo hicho kununua baadhi ya fenicha, vifaa, na vitendea kazi ikiwemo vifaa vya maabara ya nishati jadidifu kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo (testing na simulation).

Kuhusu ujenzi wa Miundo Mbinu, Profesa Chacha amesema chuo kimefanikiwa kufanya ujenzi wa majengo kumi na moja (11) katika Kampasi ya Kikuletwa na yameshakamilika.