Lameck Kanyong ala kiapo Mashujaa

LICHA ya kukabiliana na ushindani mkali wa namba katika kikosi cha Mashujaa FC, kipa Lameck Kanyonga bado ana imani atapata nafasi ya kucheza na hawezi kuikimbia changamoto hiyo.

Kanyonga amejikuta katikati ya ushindani mzito dhidi ya Erick Johola na Suleman Munthary tangu aliposajiliwa Mashujaa misimu miwili iliyopita akitokea Mbeya City.

Msimu huu, Johola amekuwa namba moja akianza mechi saba akiondoka na ‘clean sheets’ sita, huku Kanyonga akiwa  namba mbili na kuishia kwenye benchi katika mechi zote tisa.

Akizungumzia hali hiyo, Kanyonga ameliambia Mwanaspoti kuwa hatishwi na ushindani wa namba kwani anachozingatia ni kujiweka fiti ili akipata nafasi aonyeshe uwezo na kuisaidia timu.

KANYO 01

“Kila sehemu kuna ushindani. Wachezaji mnapokuwa zaidi ya mmoja lazima kuwe na ushindani, hivyo basi muhimu kwangu ni kujiweka sawa muda wowote nitakapopata nafasi niisaidie timu na kuonyesha ubora wangu,” amesema.

KANYO 02

Alisisitiza kuwa ataendelea kutumikia mkataba huku akifungua milango kwa timu zitakazomtaka kumalizana na Mashujaa FC.

“Bado niko ndani ya mkataba na Mashujaa. Bado ni mchezaji wa hii timu, na sina ofa yoyote kwa sasa, lakini itakapotokea timu ikanihitaji, basi ni mazungumzo tu ya pande tatu mimi, waajiri wangu na timu itakayonihitaji,” amesema.

Pamoja na changamoto hiyo, nyanda huyo amesema uwepo wake Mashujaa umemkomaza na kumfundisha vitu vingi ambavyo vimemsaidia katika safari ya soka, huku akisisitiza kuwa anafurahia kuwa ndani ya kikosi hicho.

“Msimu huu tumejiandaa na tumedhamiria kufanya vizuri zaidi katika ligi. Timu iko tayari na mimi binafsi bado napambania nafasi yangu, kwa majaliwa yake Mungu nikipata nafasi naamini nitafanya vizuri kwa sababu naamini katika uwezo wangu,” amesema