Maandamano ya ‘Gen Z’ yasababisha vifo maofisa usalama 14 Iran

Iran. Takribani Maofisa 14 wa usalama wamefariki dunia tangu kuanza kwa maandamano ya vijana nchini Iran.

Maandamano hayo ya vijana maarufu ‘Gen Z’ yaliyoanza Desemba 28, 2025, yamekuwa yakishinikiza mabadiliko katika mfumo wa uendeshaji wa nchi ili kukabililiana na changamoto zao na taifa kwa ujumla  ikiwemo ukosefu wa ajira na hali ngumu ya ya maisha.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka mashirika ya haki za binadamu, imeelezwa kuwa takribani vifo vya watu wasiopungua 62, vimeripotiwa tangu kuanza kwa maandamano hayo wakiwemo maafisa wa usalama 14 na waandamanaji 48.

Imeelezwa kuwa Idadi kubwa ya maofisa hao wamefariki kwenye mapigano baina yao na waanandamaji kwenye maeneo ya miji ya Taifa hilo hususani nyakati za usiku.

“Maandamano yamesababisha changamoto zaidi ingawa awali yalilenga kufikisha ujumbe wa hali ngumu ya uchumi,”imeelezwa.

Athari hizo zimeilazimu serikali kuchukua hatua zaidi ili kutuliza waandamaji ikiwemo kuzima intaneti na mitandao ya simu kama sehemu ya kupunguza uwezekano wa mawasiliano baina ya vijana ambao wamekuwa wakihamasishana.

Mbali na kuzima mitandao serikali hiyo pia imezuia safari za ndege kuingia na kutoka nchini hadi itapotolewa taarifa.

 Viongozi wa Ufaransa, Uingereza na Ujerumani wametoa taarifa ya pamoja jana Ijumaa wakilaani  mauaji ya waandamanaji na kuwasihi mamlaka ya Iran kudhibiti vurugu.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa (UN), Stephane Dujarric ameeleza kuwa umoja huo umesikitishwa na vifo vya watu.

“Watu wote, popote duniani wana haki ya kuandamana kwa amani, na serikali zina jukumu la kulinda haki hiyo na kuhakikisha kwamba haki hiyo inaheshimiwa,” amesema.

Rais wa Marekani, Donald Trump ametoa onyo kwa viongozi wa Iran akiwataka kuaacha kuwaua waandamaji kwani haitasita kuingilia iwapo serikali ya Irani itashindwa kudhiti ghasia hizo kwa kuzingatia misingi ya ubinadamu.

Imeandaliwa na Elidaima Mangela kwa msaada wa mitandao.