Dar es Salaam. Jumla ya wagonjwa 170 wamefanyiwa upasuaji wa kutengenezewa mishipa ya kuchuja damu katika Hospitali ya Muhimbili tawi la Mloganzila tangu kuanza kwa huduma hiyo mwaka 2023.
Huduma hii ilianza mwaka 2023 hospitalini hapo kwa ushirikiano wa wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi, ili kuwezesha utoaji wa huduma ya uchujaji wa damu kwa muda mrefu kwa watu wenye matatizo ya figo kwa kuweka mishipa hiyo ndani ya mwili wa mgonjwa tofauti na ilivyokuwa awali.
Hayo yameelezwa na Daktari bingwa wa upasuaji wa Mloganzila David Antasamu kuwa huduma hiyo huondoa gharama za kubadilisha mipira mara kwa mara kwa wagonjwa wa figo wanaohitaji kuchujaji damu.
Dk Antasamu amesema mishipa hiyo ni nguzo muhimu katika tiba ya wagonjwa wa figo wanaohitaji huduma ya uchujaji wa damu, kwani huokoa maisha kwa kuhakikisha uchujaji wa damu unafanyika kwa usalama, na kupunguza hatari ya maambukizi kwa wagonjwa hao.
“Tumefanya oparesheni hii kwa wagonjwa 170 tangu 2023, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nje na ndani ya nchi, ili kutengeza mishipa maalumu ya kuchuja damu,” amesema Dk Antasamu.
“Mishipa hii humpa mgonjwa uhuru wa kuendelea na shughuli zake bila changamoto ikiwemo kuvaa nguo anazotaka na kuoga mwili mzima kwa kuwa hujificha chini ya ngozi, tofauti na ile inayokuwa juu ya ngozi,” ameongeza.
Ameongeza kuwa mishipa hiyo pia huondoa uwezekano kwa mgonjwa wa figo kupata maambukizi kwa urahisi.
Dk Antansamu pia amesema aina hiyo ya mishipa, hutoa kiwango cha juu zaidi cha damu wakati wa uchujaji wa damu hivyo kuongeza ufanisi pindi mgonjwa anapokuwa kwenye mashine.
Ameongeza kuwa uwepo wa huduma hiyo ndani ya hospitali hiyo umeondoa adha kwa wagonjwa kulazimika kusafiri au kusubiri kwa muda mrefu.