Nchi tatu kujadili mustakabali uchumi wa buluu Zanzibar

Zanzibar. Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kushirikiana na shirika la Ascending Africa kupitia Mradi wa Jahazi, imetangaza rasmi ujio wa Mkutano wa Kikanda wenye lengo la kukabiliana na uvuvi haramu na kukuza uchumi wa buluu.

Mkutano huu wa siku tatu utafanyika kuanzia Januari 26 hadi 28, 2026, na utakutanisha serikali, taasisi za kikanda, wadau, wataalamu wa bahari, na washirika wa maendeleo kutoka nchi za Mauritius, Kenya, Tanzania na Zanzibar.

Lengo kuu la mkutano huu ni kuimarisha uongozi wa Afrika katika usimamizi wa bahari, kuendeleza uchumi wa buluu unaozingatia uendelevu, na kuimarisha hatua za pamoja za kukabiliana na Uvuvi Haramu katika ukanda wa Bahari ya Kusini-Magharibi mwa Bahari ya Hindi.

Ushirikiano huu unaakisi vipaumbele vya pamoja vya nchi za Kusini-Magharibi mwa Bahari ya Hindi ambazo zinakabiliwa na changamoto katika matumizi endelevu ya rasilimali za baharini, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabianchi, na ustawi wa jamii za pwani.

Kupitia Mkutano wa Blue Voices (Sauti za Buluu) 2026, nchi washiriki zinalenga kujenga mwitikio wa kikanda unaojikita katika ushirikiano wa dhati, uwazi wa mifumo ya usimamizi wa bahari, na utekelezaji wa sera, sheria na mikakati ya bahari.

Mkutano huu utaendeshwa chini ya kaulimbiu ya “Bahari Moja, Sauti Moja (One Ocean, One Voice)”, ikisisitiza ukweli kwamba bahari ya ukanda huo ni rasilimali ya pamoja inayohitaji maamuzi ya pamoja na hatua shirikishi. Kaulimbiu hii pia inaakisi dira ya muda mrefu ya Serikali ya Zanzibar ya kuitumia bahari kama nguzo kuu ya maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na kimazingira.

Akizungumza kuhusu mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ya Zanzibar Kapteni Hamad Bakar Hamad, alisema “Zanzibar imejizatiti kushirikiana kwa karibu na nchi jirani katika ukanda wa Kusini-Magharibi mwa Bahari ya Hindi kulinda bahari yetu ya pamoja”

Kapteni Hamad alisema ushirikiano wa kikanda ndio msingi wa kulinda rasilimali za baharini na kuhakikisha ustawi wa jamii zinazotegemea bahari na kusisitiza kuwa mkutano wa Blue Voices 2026 ni jukwaa muhimu la kuimarisha mshikamano wa kikanda, kuendeleza suluhu za vitendo, na kuongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya uvuvi haramu.

Kwa upande wake, Michael Mallya, Msemaji wa Mradi wa Jahazi, alisema kuwa Mkutano wa Blue Voices 2026 ni hatua muhimu katika kuinua uongozi wa Afrika katika masuala ya usimamizi wa bahari.

“Mkutano huu unaashiria mwanzo wa sura mpya katika usimamizi wa bahari Afrika Mashariki na Ukanda wa Kusini-Magharibi mwa Bahari ya Hindi kwa Ujumla. Uvuvi haramu hustawi pale mifumo inapokuwa imegawanyika na ushirikiano ukiwa dhaifu,” amesema Mallya