Pamba yazindua jezi baada ya miezi mitano

HATIMAYE Klabu ya Pamba jiji ya Mwanza imezindua rasmi jezi za msimu wa  2025/2026 na uuzaji wake utaanza leo katika mkoa wa Mwanza, baada ya subira ya mashabiki ya takribani miezi mitano tangu Ligi Kuu Bara ilipoanza Septemba 17.

Pamba imezindua uuzaji wa jezi hizo  Mwanza, leo Januari 10, 2026, katika duka lililopo mtaa wa Misheni, jijini humo ambapo zitapatikana kwa Sh30,000.

Jezi hizo zenye rangi ya kijani (nyumbani), nyeupe (ugenini) na bluu (mbadala) zinatengenezwa na mdhamini mkuu wa klabu hiyo, kampuni ya Jambo.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo katika mkutano na waandishi wa habari, Ofisa Habari wa Pamba Jiji, Moses William amekiri kuchelewesha mauzo ya jezi hizo, lakini akaanika sababu za ucheleweshaji huo kwamba ni mahitaji ya ubora utakaokidhi kiu ya mashabiki.

“Miongoni mwa akenda ambazo zilichelewesha kusaini mkataba kati yetu na Jambo ilikuwa ni watupe kwanza design (ubunifu) ya jezi ambavyo zitakuwa, kwa sababu tulikuwa tunaogopa kule tulikotola halafu msimu huu tukatoa jezi ambazo ni mbaya ama watu wakaona ni bora zile za msimu jana,” amesema William.

Ameongeza kuwa: “Watengenezaji wetu walituumiza kichwa kwenye hii jezi, watu wanaweza kuona kuwa tulichelewa kutoa jezi jambo ambalo ni kweli, lakini tulihitaji kitu ambacho ni bora. Sasa hivi mtu yeyote ukimuonyesha kwamba tulichokuwa tunakisubiria ndicho hiki, ina hadhi ya kusubiriwa.”

ofisa huyo amesisitiza kuwa klabu hiyo kwa kushirikiana na watengenezaji, wasambazaji na waauzaji wa jezi hizo wataanza msako wa maduka yanaouza jezi feki kwa kati ya  Sh10,000 hadi Sh15,000, kwani tayari taarifa zao wanazo.

Kiongozi Mkuu wa chapa na nembo ya Jambo, Nickson George amesema kwa sasa jezi hizo zinauzwa katika duka moja pekee Mwanza na yeyote atakayeuza tofauti na msambazaji huyo atachukuliwa hatua za kisheria.

George amesema tayari wanafahamu uwepo wa jezi feki ambazo zimeshaanza kuzunguka mitaani takribani mwezi sasa, na maduka yanayouza jezi hizo, hivyo, kwa kushirikiana na wanasheria wa klabu watawakamata.

“Tumeshakubaliana tuko tayari kwa ajili ya kuanza kufanya upekuzi wa maduka yote ambayo tunajua wanauza jezi feki za Pamba ambao hatuwatambui na wanafanya kinyume na sheria za nchi, na wanaihujumu Pamba inashindwa kuingiza mapato,” amesema George.

Akizungumzia sababu za kuchelewesha uuzwaji wa jezi za Pamba, George amesema; “Sisi kama wadhamini wakuu wa Pamba tumeamua kuja mbele yenu leo hii na kutangaza rasmi ujio wa jezi hizi na kuwatangazia kwamba zimeanza kuuzika kuanzia Januari 10, 2026 na kuendelea na sehemu ya kwanza ambayo utakuwa unazipata katika maduka ya Ommy Fashion.”

Kwa upande wake, muuzaji wa jezi hizo, Omary Ramadhan amesema ameamua kuingia mkataba wa kuuza jezi za Pamba Jiji baada ya kuvutiwa na ubora wake, huku akiwahamasisha wapenzi wa soka Kanda ya Ziwa kuzichangamkia.

“Kilichonivutia ni kwamba Pamba ni timu kubwa na ina wapenzi wengi, na pia uzalendo lazima tupende kwanza cha kwetu. Jezi ni nzuri, halisi, ina ubora, hivyo imenivutia, tunataka watu wavae vitu vizuri vyenye ubora na wavutie,” amesema