Rais Samia aeleza sababu za kumteua Profesa Kabudi

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, ameweka wazi sababu za kumteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu (Kazi Maalumu).

Kabla ya uteuzi, Profesa Kabudi alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Rais amesema uamuzi huo umetokana na mahitaji mapya ya uendeshaji wa Serikali katika mazingira ya siasa za kimataifa na usimamizi wa juu wa masuala nyeti ya Taifa.

Ikumbukwe kuwa Januari 8, 2026, Rais Samia alifanya mabadiliko madogo katika Baraza lake la Mawaziri, pamoja na teuzi nyingine, alimteua Profesa Kabudi kushika wadhifa huo mpya huku nafasi yake ya awali ikichukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo, Paul Makonda.

Mabadiliko ya wateule hao wanaotarajiwa kuapishwa Jumatatu, Januari 13, mwaka huu Ikulu jijini Dodoma, yalielezwa kulenga kuongeza ufanisi na kuendana na kasi ya mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ndani na nje ya nchi.

Akizungumza leo Jumamosi, Januari 10, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwapongeza wanamichezo wa Tanzania waliofanya vizuri na kulitangaza taifa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, Rais Samia amesema tukio hilo pia lilikuwa fursa ya kumuaga rasmi Profesa Kabudi katika Wizara ya Michezo na kumkaribisha katika majukumu mapya Ikulu.

“Katika jambo jingine ambalo limeingia leo hapa, shughuli hii ni ya kumuaga pia Profesa Kabudi kutoka Wizara ya Michezo na kuja kwangu Ikulu. Sio kwamba tunabadilisha tu, bali ni kwa sababu ya kuendana na siasa za dunia zinavyokwenda. Kuna nchi na taasisi zinazolitazama taifa letu kwa jicho chanya, na zipo pia zinazolitazama kwa jicho hasi,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa mazingira hayo yanahitaji Ikulu kuwa na wasaidizi wenye upevu wa hali ya juu, maarifa mapana na uzoefu mkubwa wa kitaifa na kimataifa, pamoja na uwezo wa kujieleza kwa ufasaha na kufikisha hoja kwa uelewa mpana.

“Pale Ikulu nahitaji akili iliyopevuka, yenye maarifa mapana, uzoefu mkubwa, na mtu ambaye yuko vizuri kwenye kujieleza na kueleza jambo likaeleweka. Nimepiga picha serikalini kwangu kote, nikasema Profesa Kabudi atanifaa,” amesisitiza Rais.

Rais Samia amesema hivi karibuni amefanya pia uteuzi wa washauri wake wakuu, akiwemo aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyemteua kuwa mshauri wake katika masuala ya uchumi na miradi ya maendeleo.

Dk Mpango anafahamika kwa uzoefu wake mkubwa katika masuala ya uchumi, fedha na mipango ya maendeleo, akiwa amewahi kuhudumu kama Waziri wa Fedha na baadaye Makamu wa Rais, nafasi iliyompa uelewa mpana wa uendeshaji wa Serikali na mahusiano ya kimataifa ya kiuchumi.

Pia, Rais Samia amesema amemteua aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa mshauri wake katika masuala ya kijamii.

Amesema Majaliwa ambaye aliyeongoza shughuli za Serikali kwa miaka 10, anao uzoefu mkubwa katika kushughulikia masuala ya jamii, utawala wa umma na usimamizi wa utekelezaji wa sera za Serikali hadi ngazi za chini.

“Sasa vile vichwa viwili vikubwa vinahitaji mtu aliyetulia, mtulivu na anayeweza kushughulika nao vizuri,” amesema Rais, akieleza umuhimu wa kuwa na mtu mwenye hekima na uwezo wa kusimamia mijadala na majadiliano ya ngazi ya juu kwa utulivu na busara.

Katika maelezo yake, Rais Samia ametania kwa kueleza kuwa nafasi ya ushauri inapopata mtu makini wakati mwingine wanaweza kujibu mambo kwa haraka, hali inayoweza kuleta changamoto, lakini Profesa Kabudi ana uwezo wa kwenda nao sambamba kwa utulivu na weledi.

“Hawa watoto wangu hawa maana wanaweza kujijibu tu, ikaja kesi. Lakini Profesa anaweza akaenda nao vizuri sana. Kwa hiyo hizo ndizo sababu zilizonifanya nimchukue Profesa Kabudi kuja kwangu Ikulu anisaidie kazi hizo,” amesema.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa uamuzi wa kumhamisha Profesa Kabudi haukuwa dalili ya kutokuwa na imani na wizara aliyokuwa akiiongoza, bali ni sehemu ya mkakati wa kupanga vyema rasilimali watu serikalini. Amesema Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo sasa ipo mikononi mwa viongozi wanaoendana na nguvu na mahitaji ya sekta hiyo, hususan vijana.

“Nilijipa moyo kwamba Mwana FA (Hamis Miwnjuma-Naibu Waziri) na Makonda wanaweza kuiendesha wizara vizuri kwa sababu ni wizara ya vijana, na wao zile hekaheka wanazimudu. Ni vijana kwa vijana wenzao,” amesema Rais.

Amesema endapo angeamua kumchagua Makonda kama mshauri wake Ikulu, baadhi ya watu wangeweza kuhoji uamuzi huo, lakini katika wizara inayowahusu vijana, Makonda anaeleweka na kukubalika miongoni mwao, huku Mwana FA naye akiwa na ushawishi mzuri kwa wadau wa sekta ya michezo na sanaa.

Katika hatua nyingine Rais Samia amesisitiza juu ya Watanzania kuendelea kudumisha amani na mshikamano ili nchi iendelee kufanya vema kimataifa.