RAMIA ABDIWAWA ATOA PONGEZI NA USHAURI KWA TNCC KATIKA ZITF

::::::::

 Waziri Mstaafu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa ameipongeza Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) kwa uongozi wake wenye mwelekeo chanya na mchango wake mkubwa katika kukuza biashara na diplomasia ya kiuchumi kupitia Maonesho ya 12 ya Biashara ya Kimataifa ya Zanzibar (Zanzibar International Trade Fair – ZITF) yanayoendelea visiwani Zanzibar.

Waziri Mstaafu huyo alitoa pongezi na ushauri huo wakati wa ziara yake katika banda la TNCC, ambapo alipata fursa ya kujionea huduma, taarifa na fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zinazoratibiwa na Chemba hiyo kwa wafanyabiashara wa ndani na wa kimataifa.

Akizungumza mara baada ya kutembelea banda hilo, Waziri Mstaafu, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa alisema maonesho ya ZITF yameandaliwa kwa viwango vya juu, yakionesha dhamira ya dhati ya Serikali na taasisi zake katika kuimarisha mazingira ya biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

“Maonesho haya ni jukwaa muhimu sana kwa wafanyabiashara kukutana, kubadilishana uzoefu na kujenga mitandao ya kibiashara. TNCC imeonesha uongozi madhubuti na weledi mkubwa katika kusimamia maslahi mapana ya sekta binafsi,” alisema Waziri Mstaafu huyo.

Aidha, alishauri waandaaji wa ZITF kuendelea kuboresha zaidi maonesho hayo kwa kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara na wawekezaji wa kimataifa, pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika uwasilishaji wa fursa za biashara ili kuyaweka maonesho hayo katika ushindani wa kimataifa.




 *Mwisho*