KUSHINDA mechi zote tatu za First League siyo bahati mbaya kwa maafande wa Rhino Rangers ya Tabora, kwani wamedhamiria kufanya vizuri na kupanda daraja kwenda Ligi ya Championship msimu huu.
Rhino Rangers inakamata usukani wa kundi B lenye timu nane za First League, ambapo imevuna pointi tisa katika mechi tatu baada ya kushinda zote, huku ikifunga mabao nane na kuruhusu moja.
Kundi hilo lina timu za Mapinduzi FC, Endument, IAA SC, Alliance FC, Copco FC, Nkim FC, na Biashara United, ambapo Biashara United inashika mkia ikiwa inadaiwa alama tatu (-3), huku Nkim ikiwa haina pointi.
Kocha Mkuu wa Rhino Rangers, Gift Emmanuel amesema malengo ya msimu huu ni kupanda daraja, hivyo wanaiandaa timu kiufundi, kisaikolojia na kimwili kwa ajili ya kushindana ili kufikia lengo hilo.
“Kiuhalisia ni kwamba lengo letu ni kuingia Championship. Tunahitaji tuitengeneze timu iwe vizuri. Tunajiandaa vizuri kiufundi, tumewandaa wachezaji ili waweze kupata matokeo ya ushindi katika mechi zetu,” amesema Emmanuel na kuongeza:
“Baada ya mapumziko ligi imerejea na sisi tunajiandaa kwa mchezo wa Januari 10 dhidi ya Mapinduzi. Tumerudi tumejaribu kuwajenga wachezaji kisaikolojia, kiakili na kimwili ili waweze kurudi.”
Akizungumzia usajili wa dirisha dogo, kocha huyo amesema wanafikiria kuongeza wachezaji, lakini kwa sasa bado wanaendelea kufanya tathmini ili kuona maeneo ya kuyafanyia maboresho.
“Tutaangalia sehemu ambazo zina udhaifu kama zipo tutatafuta watu sahihi wa kuongeza, kiufupi tutaongeza watu lakini hatujakaa kuamua tuongeze eneo gani,” amesema.
