RAIS Samia Saluhu Hassan ameipongeza timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kwa kufika 16 bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), inayoendelea huko Morocco.
Stars iliyokuwa inashiriki mashindano hayo kwa mara ya nne ilitolewa na Morocco kwa kuchapwa bao 1-0, ingawa imeweka rekodi ikiwa ni mara ya kwanza inafika hatua hiyo kwani mara tatu iliishia makundi.
Rais Samia amesema hayo alipowaalika wanamichezo, wadau wa michezo, viongozi wa serikali na wachezaji wa zamani Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya chakula cha mchana kwa lengo la kuwapongeza.
“Mafanikio haya ni makubwa na ni fahari kwa taifa letu na ni ushahidi kwamba soka letu linaendelea kupanda viwango vya ubora barani Afrika, kwa mara ya kwanza nilikaa kwenye televisheni mwanzo hadi mwisho,” amesema Rais Samia na kuongeza:
“Siku hiyo nilikuwa nimefunga nimekaa kufutari, wakati naendelea na futari yangu tayari mechi inataka kuanza, nikakaa na kuangalia watoto wangu kazi wanayoifanya, lakini nikaondoka pale mwili wote unaniuma mlipokuwa mkipigwa na kuzuiwa.”
Rais Samia amesema anajua ni kwa nini mambo yote yaliyotokea kwa sababu tuliocheza nao ni wenyeji wa mashindano hayo, taifa lenye fedha na taifa lenye ushawishi pia, ingawa dunia nzima imeona wazi kwamba Tanzania ni wapambanaji.
“Nalipongeza pia benchi la ufundi, viongozi wa timu na wanamichezo wengine wote mliopo hapa, ni ukweli kama walivyosema walionitangulia michezo yetu imepanda, naipongeza pia timu ya kriketi kwa kufuzu Kombe la Dunia Namibia,” amesema Samia.
Pia aliipongeza timu ya Mpira wa Miguu ya Wanawake Futsal kwa kushiriki Kombe la Dunia Ufilipino na mabondia waliotwaa mikanda ya kimataifa, ikiwemo timu ya taifa ya ridhaa iliyopata medali 18, ikiwemo moja ya dhahabu, medali za fedha nne na 13 za shaba katika mashindano ya kanda ya tatu ya Afrika yaliyofanyika Nairobi Kenya.
“Tunakwenda ndugu zangu, tulikotoka sio tulipo leo, walau jina la Tanzania linasikika na kuonekana kwenye kila fani, pia nawapongeza mabondia kwa ushiriki wa mashindano ya dunia yaliyofanyika Dubai, ambapo bondia wetu mmoja alifika hatua ya 16 bora.”
Katika hatua nyingine, Rais Samia alizipongeza timu za taifa zilizofanya vizuri kwa ukanda wa Cecafa zikiwemo timu za vijana, shule, kuogelea na watu wenye ulemavu kwa kuipeperusha vyema bendera nje ya Tanzania.
Rais Samia alimpongeza mwanariadha Alphonce Felix Simbu kwa kushinda medali ya dhahabu ya Tokyo Marathon 2025, akiwa ni Mtanzania wa kwanza kutwaa dhahabu ya kimataifa na Sisilia Ginoka Panga kwa kutwaa dhahabu ya mbio za kilomita 15 zilizofanyika Sao Paulo, Brazil.
“Jitihada na nidhamu mlizozionyesha ni alama ya uzalendo wa kweli, mmeipeperusha vyema bendera yetu ya taifa la Tanzania na mmeandika historia mpya kwa taifa letu katika ulimwengu wa michezo,” amesema Samia.
Kwa upande mwingine Rais amesema Tanzania ina kazi kubwa ya kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, hivyo, maandalizi yanahitajika mapema, mshikamano wa kitaifa na ushirikiano wa karibu kati ya wadau wa michezo nchini na Serikali.
“Ni wajibu wetu sote kuhakikisha AFCON 2027, inafanyika kwa ufanisi mkubwa, kwa heshima na manufaa ya taifa letu, ni dhahiri ili tufanye vizuri hatuna budi kuwekeza katika maendeleo ya wachezaji wetu wanaohitaji mechi nyingi za ndani ili kupata uzoefu,” amesema na kuongeza:
“Nitoe rai ya ushirikiano baina ya klabu na wadau wa soka kuhakikisha Ligi zetu zinaendelea kuwa imara, shindani na pia zinawapa nafasi wachezaji wazawa kukua, tusiwarudishe nyuma ili wakue, kwani uzoefu utawaandaa vyema kushindana katika nyanja za kimataifa.”
Rais Samia amesema atahakikisha anaendelea kuboresha maslahi na posho mbalimbali kwa timu za taifa baada ya hivi karibuni kupata taarifa kuwa kulikuwa na tishio la mgomo ikiwa Misri kabla ya kwenda Morocco kwenye mechi za AFCON.
“Kwa wachezaji tunajua mnachohitaji, lakini kuhusu suala la posho zenu niwahakikishie hilo tutalifanyia kazi,” amesema Samia.
Pia, Rais alitumia nafasi hiyo kumshukuru rais wa Shirikisho la Soka Africa (CAF), Patrice Motsepe kwa kumtunuku tuzo maalumu ikiwa ni ishara ya kutambua na kuthamini mchango wake mkubwa anaoendelea kuuonyesha katika mchezo wa soka.
