KESHOKUTWA kitawaka katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza ambapo mashabiki wa Simba na Pamba Jiji watapomenyana katika mchezo wa kirafiki ikiwa ni sehemu ya kunogesha sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.
Mchezo huo wenye lengo la kuendeleza umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa mashabiki wa Simba na Pamba waliopo katika Mkoa wa Mwanza, utachezwa Jumatatu Januari 12, 2026 kuanzia saa 7 mchana katika Uwanja wa Nyamagana.
Ofisa Michezo wa Jiji la Mwanza, Mohamed Bitegeko amesema klabu hizo mbili zina mashabiki wengi ambao wataunganishwa na mchezo huo, hivyo watachuana kunogesha sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar hizo.
”Mechi hii itatumika kuonyesha kuwa mpira wa miguu ni chombo cha amani, utulivu na masikilizano, na siyo chanzo cha kutengana na kubaguana. Pia, kukuza michezo na utalii wa michezo ndani ya mkoa wetu wa Mwanza,” amesema Bitegeko.
Amesema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda atanogesha mchezo huo, huku akisisitiza kuwa mbali na Simba na Pamba Jiji, mchezo huo utawaunganisha mashabiki wote wa soka mkoani humo.
Amesema katika maandalizi ya mchezo huo, wachezaji wote wakongwe waliowahi kuzitumikia timu za Simba na Pamba katika kipindi cha nyuma wanaoishi mkoani Mwanza wameshirikishwa pia.
”Kwa niaba ya kamati ya maandalizi, napenda kusema wazi kuwa Mwanza itakuwa mfano wa kuigwa katika kuonyesha kuwa Simba na Pamba wanaweza kushindana kwa heshima na kuishi kama ndugu,” amesema Bitegeko.
Katibu wa Simba Mkoa wa Mwanza, Philbert Kabago ametamba kuwa wamejipanga vizuri kushinda mchezo huo na kupoza machungu ya timu yao kutolewa kwenye michuano ya Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar.
”Tunao wachezaji waliocheza Simba kwa mafanikio makubwa siku hiyo watacheza, tunaamini tutaibuka na ushindi kwa sababu tunao nyota kama Amir Maftah, Juma Amir, Msonga Rashidi, na Eric Majaliwa watakaotoa burudani kwa mashabiki watakaojitokeza,” amesema Kabago.
Mwakilishi wa mashabiki wa Pamba, Moses William amesema: “Msisitizo wetu ni uleule malengo ni mahusiano lakini mahusiano yatakuwa mazuri zaidi mara baada ya mashabiki wa Pamba kuwachakaza wenzetu wa Simba. Tupo tayari, tumejipanga sawasawa.”

