VIONGOZI wa Nyassa Big Bullets ya Malawi wameweka msimamo mkali baada ya kukataa ombi la Simba la kumtaka winga Chikumbutso Salima (21), kwa ajili ya majaribio ya wiki mbili.
Hatua hiyo imekuja baada ya Simba kuonyesha nia ya kumuangalia kwa karibu winga huyo chipukizi kabla ya kufanya uamuzi wa kumsajili moja kwa moja katika dirisha hili dogo la usajili.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Nyassa Big Bullets, uongozi wa timu hiyo umeeleza kuwa haupo tayari kumuachia mchezaji wao kwa majaribio, bali wako tayari kufanya biashara ya moja kwa moja endapo Simba itakuwa tayari kukidhi masharti ya uhamisho wa jumla.
Msimamo huo umeelezwa kuwa ni sera ya klabu katika masuala ya uuzaji wa wachezaji wake muhimu.
Chikumbutso amekuwa akionyesha kiwango cha juu ndani ya Ligi Kuu Malawi akifunga mabao 14, jambo lililovutia macho ya klabu mbalimbali Afrika.
Kasi, uwezo wa kupiga chenga pamoja na mchango wake katika ufungaji wa mabao ni miongoni mwa sifa zilizoifanya Simba kumuona kama chaguo sahihi la kuimarisha safu ya ushambuliaji.
Hata hivyo, menejimenti ya mchezaji huyo inaendelea kufanya juhudi za kuwashawishi Nyassa Big Bullets wakubali kumuachia winga huyo kwa majaribio ya muda mfupi kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa.
Menejimenti inaamini kuwa majaribio hayo yatampa mchezaji nafasi ya kuonyesha uwezo wake na pia kuongeza thamani yake sokoni.
Kwa upande wa Simba taarifa zinaeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo bado unafanya tathmini ya kina ili kuamua kama wataingia kwenye mazungumzo ya uhamisho wa moja kwa moja au wataachana kabisa na dili hilo kutokana na masharti yaliyowekwa na klabu ya Nyassa Big Bullets.
Nyassa Big Bullets kwa upande wao wanaamini Chikumbutso ni sehemu muhimu ya mipango yao, jambo linalowafanya kuwa wagumu kumwachia bila kupata faida inayolingana na thamani yake.
