Suala la posho Stars lilivyomshtua Rais Samia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa alishtushwa na taarifa za mgomo wa wachezaji wa Taifa Stars kabla ya Fainali za AFCON 2025 kutokana na madai ya posho.

Akizungumza katika hafla ya kuipongeza Taifa Stars, Rais Samia amesema kuwa taarifa hizo hakuzipokea vizuri lakini bahati nzuri mgomo huo haukufanyika.

“Jicho letu liwe kwa vijana wetu. Kuwafanyisha mazoezi lakini pia vijimaslahi vyao. Tarehe gani ile nilikuwa nimekaa mara paap napokea taarifa kutoka vyombo vyangu vya serikali, wachezaji wamegoma kwenda Morocco kutoka Misri.

“Nini? Kiposho kidogo hakitoshi. Mie Mungu wangu weeh! Makonda (Paul) haya mnafanyaje kuhusu hili? Sitaki vijana kule wawe wameshuka morali kwa namna yoyote ebu changamka basi.

“Mara paap namsikia Makonda anatangaza dau la 200 (milioni), nikasema yes, hivyohivyo,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema serikali itajitahidi kuhakikisha wachezaji wa Taifa Stars wanapata stahiki zao kwa wakati.

“Kwa wachezaji tunajua suala la viposho vyenu, tutalifanyia kazi,” amesema Rais Samia.

Mbali na suala la posho, Rais Samia amesema kuwa serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo, kuvutia wawekezaji wa michezo na kutoa ushirikiano kwa wanamichezo ili sekta hiyo ipige hatua.

Akizungumzia fainali za AFCON 2027 ambazo Tanzania itakuwa ni miongoni mwa nchi tatu wenyeji, Rais Samia ameshauri Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania na Baraza la Michezo la Taifa kwa kushirikiana na klabu za soka, kuhakikisha wachezaji wazawa hapa nchini wanapata nafasi ya kutosha ya kucheza ili wapate uzoefu wa kuwawezesha kufanya vizuri katika fainali hizo.

Mbali na Taifa Stars, Rais Samia pia amewapongeza wanariadha na mabondia wa Tanzania waliofanya vizuri kimataifa pamoja na timu za taifa za michezo ya Futsal na Kriketi.