MAAFANDE wa Tanzania Prisons wameanza mazungumzo na Singida Black Stars kwa ajili ya kupata saini ya Ayoub Lyanga kwa mkopo katika dirisha hili dogo la usajili ikiwa ni pendekezo la Kocha Mkenya Zedekiah ‘Zico’ Otieno.
Awali ilielezwa mabosi wa Singida walikuwa na mpango wa kumtoa Lyanga kwa mkopo katika dirisha kubwa la usajili, ingawa dili hilo liligonga mwamba, japo kwa sasa huenda likakamilika baada ya maafande wa Prisons kufungua mazungumzo rasmi.
Taarifa kutoka Prisons, zinaeleza mabosi wa timu hiyo wamefungua mazungumzo ya kupata saini ya nyota huyo ambaye tayari amerejea katika kikosi hicho, ambacho kilikuwa kinashiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026, huko visiwani Zanzibar.
“Mazungumzo yanaendelea vizuri kwa ajili ya kupata saini ya nyota huyo, tunahitaji maboresho makubwa hasa katika eneo la ushambuliaji kutokana na ripoti ya benchi la ufundi, tageti ni kupata nyota wanne hadi watano,” kilisema chanzo hicho.
Katika mechi saba za Ligi Kuu Bara ilizocheza Prisons hadi sasa, safu ya ushambuliaji ya timu hiyo imefunga mabao matatu tu, jambo linalochangia uongozi wa kikosi hicho kuingia sokoni haraka dirisha hili dogo ili kuliongezea nguvu eneo hilo.
Lyanga aliyejiunga na kikosi hicho Julai 9, 2024, akitokea Azam, amekuwa na kipindi kigumu cha kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, tangu ujio wa winga, Mgambia Lamine Jarjou, aliyejiunga msimu huu akitokea Grenoble Foot 38 ya Ufaransa.
