Tanzania imemaliza katika nafasi ya 11 kwenye mashindano ya dunia ya mbio za nyika zinazoendelea Tallahassee, Florida nchini Marekani kwa upande wa relay mchanganyiko, huku Australia ikitwaa medali ya dhahabu baada ya kuibuka mshindi.
Katika mbio hizo Tanzania ilikuwa inaundwa na wanariadha Daniel Sinda, Elizabeth Ilanda, Ambrosi Amma na Regina Mpigachai ambapo imemaliza kwa muda wa dakika 24:11.
Nafasi ya kwanza imeshuudiwa ikienda kwa Australia ambayo timu yake ilikuwa inaundwa na Olli Hoare, Linden Hall, Jack Anstey na Jessica Hull ambayo imemaliza mbio hizo kwa muda wa dakika 22:23, ikiboresha medali ya shaba iliyoipata 2023.
Nafasi ya pili imekwenda kwa Ufaransa ilihali ya tatu Ethiopia, huku Kenya, mabingwa mara nne wa mashindano hayo ikimaliza nafasi ya tano na kushindwa kupata medali.
Mbio zingine ambazo tayari zimekimbiwa ni za wanawake chini ya umri wa miaka 20, nafasi ya kwanza na ya pili ikienda kwa Waethiopia, Marta Alemayo na Wosane Asefa huku Charity Cherop wa Uganda akimaliza nafasi ya tatu. Katika mbio hizo Tanzania haikuwa na mwakilishi.
Tumaini la Tanzania kurudi na medali sasa limebaki kwa wanariadha ambao watakimbia kilomita 10 ambao ni Gabriel Geay, Benjamin Fernandi, Emmanuel Dinday, John Wele na Inyasi Sule.
