:::::::::::
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema TRA itaendelea kupambana na watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ukwepaji wa kodi kwa kudhibiti mianya inayotumika kukwepa kodi.
Akiahirisha kikao cha tathmini ya utendaji kazi wa TRA kwa kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika kwa muda wa wiki moja kwenye ukumbi wa mikutano wa Kimataifa AICC jijini Arusha Desemba 09.01.2026 Kamishna Mkuu Mwenda amesema hawatawavumilia wakwepa kodi wowote.
Amesema miongoni mwa hatua watakazochukua ni kuimarisha mipaka, kuzuia magendo na kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa jamii sambamba na elimu ya magendo.
Sambamba na kupambana na wakwepaji kodi Kamishna Mkuu amesema wamejipanga kuongeza wigo wa kodi kwa kusajili walipakodi wapya wakiwemo wafanyabiashara ambao bado hawajaingia katika mifumo ya kulipa kodi.
Amesema TRA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu kama ilivyo jadi yake kwa kuwasikiliza walipakodi, kuwezesha biashara zao na kutatua changamoto zinazowakabili.
“Natamani siku moja TRA iisaidie nchi kujitegemea, lengo lililobaki katika awamu mbili za mwisho ni Sh. Trilioni 17.962 ambalo naamini tutalitimiza” amesema Bw. Mwenda.


