WAKATI bingwa wa kihistoria wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC ikijiandaa kuikabili Yanga katika fainali ya michuano hiyo, kuna nyota watatu wametengwa kwa kupewa programu maalumu.
Nyota hao ni Nassor Saadun, Abdul Suleiman ‘Sopu’ na Sadio Kanoute ambao wote wapo katika hatua ya kurudi uwanjani wakitokea kuuguza majeraha.
Kocha Florent Ibenge ameamua kuwatenga nyota hao ambao wamekuwa wakicheza kikosi cha kwanza na kuwakabidhi kwa mtaalamu wa tiba za viungo, Hassen Guemri.
Mwanaspoti limewashuhudia nyota hao wakati wa mazoezi ya timu hiyo ikijiandaa na mechi ya fainali dhidi ya Yanga, wao wakifanya pembeni wakiwa na Guemri katika kipindi hiki wakipambana kurejea rasmi uwanjani wakitokea kuuguza majeraha.
Sopu ambaye alikuwa miongoni mwa nyota waliounda kikosi cha Taifa Stars kilichokwenda Morocco kushiriki AFCON 2026, baadaye alichomolewa baada ya kuripotiwa ni majeruhi.
Kanoute ambaye alicheza mechi ya kwanza Kombe la Mapinduzi dhidi ya Singida Black Stars, hakuonekana tena zilizofuata dhidi ya Mlandege, URA na Simba baada ya kupata majeraha, huku Saadun aliyeivuruga Simba katika Mzizima Dabi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Desemba 7, 2025, pia hajacheza mechi yoyote ya Mapinduzi.
