Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limeweka wazi kuwa litawafuatilia wanafunzi 19 walioandika matusi kwenye mitihani ya upimaji ya kitaifa ya darasa la nne na kidato cha pili iliyofanyika 2025 na kuhakikisha shule zinawachukulia hatua za kinidhamu.
Hatua hiyo inakuja kufuatia kukithiri kwa vitendo vya watahiniwa kuandika matusi kwenye mitihani, ambapo imeelezwa kuwa hawataishia kufutiwa matokeo yao bali watafuatiliwa na kuchukuliwa hatua zaidi.
Katika matokeo ya mtihani upimaji wa kitaifa wa darasa la nne uliofanyika Oktoba 2025, imebainika wanafunzi wanane wameandika matusi kwenye mitihani, wakati kwa upande wa kidato cha pili waliofanya kosa hilo ni 11.
Akizungumza leo Januari 10,2026 Katibu Mtendaji wa Necta, Profesa Said Mohamed amesema ufuatiliaji huo utafanyika kwa kuandika barua kwa wakuu wa shule husika za wanafunzi hao kwa kuwa bado wako kwenye mfumo wa shule.
“Tutaandika barua kwa mamlaka zao ikiwemo wakuu wa shule na bodi za shule au kamati za shule kwa ngazi ya shule za msingi, ikiwahusisha wazazi kuchukua hatua ili kuhakikisha suala la kuandika matusi linakomeshwa kabisa.
“Ukiangalia takwimu zetu, ni kweli sasa tunaanza kuona matusi kwa wanafunzi wa ngazi ya darasa la nne, mwaka jana tulikuwa na wanafunzi watano ila mwaka huu wamefika wanane, kwa sababu hawa bado wako kwenye mfumo wa elimu tutachukua hatua,” amesema Profesa Mohamed.
Mtaalamu wa elimu na malezi, Asha Mwakalukwa, amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa inaonyesha tatizo hilo halichukuliwi kama kosa dogo, bali ni ishara ya mmomonyoko wa maadili kwa watoto.
Amesema kuandika matusi katika mitihani ni dalili ya changamoto kubwa ya malezi na mazingira yanayomzunguka mtoto, ikiwemo matumizi holela ya mitandao ya kijamii na lugha chafu kwenye jamii.
“Badala ya kuwaadhibu kwa kuwafuta matokeo pekee, ufuatiliaji shuleni na ushirikishwaji wa wazazi utasaidia kutambua chanzo cha tabia hiyo na kuirekebisha mapema,” amesema.
Sambamba na hilo, Necta imefuta matokeo ya wanafunzi 41 wa darasa la nne na 29 wa kidato cha pili waliofanya udanganyifu kwenye mitihani hiyo ya upimaji.
Yaliyojiri kwenye matokeo
Katika mtihani wa darasa la nne jumla ya wanafunzi 1,324,970 sawa na asilimia 88.91 wamefaulu kuendelea darasa la tano kwa kupata madaraja ya A,B,C na D ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.51 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2024.
Kwa upande wa kidato cha pili jumla ya wanafunzi wa shule 705,091 sawa na asilimia 86.93 wamefaulu kuendelea na kidato cha tatu kwa kupata daraja la kwanza hadi la nne ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.52 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2024.
Mwaka 2025 kwa mara ya kwanza mtihani wa kidato cha pili ulifanyika katika mikondo miwili ukihusisha mkondo wa amali ambapo matokeo yanaonesha wanafunzi wamefaulu kwa asilimia 100 katika masomo ya fani za amali za uhandisi, umeme, mitambo, magari na Tehama.
Katika masomo ya fani za amali zisizo za uhandisi ikiwemo kilimo na chakula, ukarimu na utalii, mavazi na ushonaji, michezo na sanaa za ubunifu, masomo nane kati ya 14 wanafunzi wamefaulu kwa asilimia 100.
Hata hivyo matokeo ni mabaya kwa somo la Leather Goods and Footwear ambapo wanafunzi watatu pekee kati ya 20, sawa na asilimia 15 ndiyo wamefaulu.
Suala la wanafunzi waliosajiliwa kutofanya mtihani limeendelea kuonekana katika mwaka wa masomo 2025 ambapo watahiwa 77,689 wa kidato cha pili sawa na asilimia 8,74 hawakufanya mtihani huo licha ya kusajiliwa.
Kwa upande wa darasa la nne walisajiliwa 1,583,686 lakini wanafunzi 93,309 sawa na asilimia 5.89 hawakufanya mtihani huo wa upimaji.
