Geita. Wananchi mkoani Geita walioathiriwa na vurugu wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2025, wamejitokeza mbele ya Tume ya uchunguzi na kutoa maoni yao.
Wakizungumza leo Jumamosi Januari 10, 2026, mbele ya Mjumbe wa Tume hiyo ambaye ameongoza jopo la Tume hiyo kwa Mkoa wa Geita, Balozi Ombeni Sefue, baadhi ya waliofika kutoa ushahidi, wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia ili kutibu majeraha yaliyosababishwa na matukio hayo.
Baadhi yao wananchi waliofika katika Ukumbi wa Nyerere uliopo viwanja vya maonyesho Manispaa ya Geita, wameeleza kupotelewa na wapendwa wao ambao waliwategemea katika maisha ya kila siku kunavyowaathiri kwa sasa na kukosa tumaini.
Balozi Ombeni Sefue (kushoto) na Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu Said Mwema wakiendelea kusikiliza wananchi waliofika kutoa ushahidi kuhusu vurugu za baada ya uchaguzi, mkoani Geita leo Januari 10,2026. Picha na Geofrey Chubwa.
Miongoni mwa makundi ya waliojitokeza kutoa maoni ni pamoja na wananchi waliofiwa na wapendwa wao, wafanyabiashara, askari, viongozi wa vyama vya siasa na watu wenye ulemavu.
Robert Paulo (56) mkazi wa Katoro ambaye ni mkulima, anasimulia namna anavyopitia wakati mgumu baada ya kufiwa na mkewe Monica Juma kufuatia kupigwa risasi na kumuachia mtoto wa miaka mitatu.
“Mke wangu tulikuwa pamoja lakini ghafla nikaambiwa amepigwa risasi na amefariki, kwa kweli nina majonzi makubwa moyoni, alikuwa mjamzito na aliniachia mtoto mdogo wa miaka mitatu, ninaumia lakini nabaki sina la kufanya,” amesema Robert
Hata hivyo, mwananchi huyo anapendekeza kuwe na mashauriano baina ya Serikali na wananchi huku akipendekeza pia vyombo vya ulinzi na usalama kuwa na utulivu katika kudhibiti vurugu ili kuepuka wasiohusika kuathiriwa tena.
“Kwa vile tumejifunza, ikitokea tena Serikali ichunguze na iwe na uvumilivu, kuwe na njia mbadala ya kutuliza vurugu wakati zinapotokea. Pia, Serikali ingetafuta namna ya kutuliza mioyo yetu tulioumizwa, kama mimi nimeachiwa mtoto mdogo wa miaka mitatu sijui namna ya kufanya,” amesema Robert.
Baadhi ya wananchi walioathiriwa na madhira yaliyosababishwa na vurugu baada ya Uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025 wakiwa katika ukumbi wa Nyerere Manispaa ya Geita kutoa maoni yao kwa tume ya uchunguzi.
Spensioza Musa ambaye ni mlemavu wa macho na mama wa watoto wanne, ameiomba Serikali kumshika mkono kwakuwa anapitia wakati mgumu baada ya kijana wake aliyekuwa tegemeo lake kufariki.
Aidha Spensioza anabainisha kuwa mtoto wake alikuwa akifanya kazi ya bodaboda, pia ndiye alikuwa tegemezi kwa familia yake.
Naye Agnes Romani (54) mkazi wa Kata ya Kalangalala Manispaa ya Geita, ambaye katika vurugu hizo kijana wake Hassan Issa (34) alifariki akitokea kununua sukari dukani na kuacha mke na watoto wawili, ameiomba Serikali kuzungumza na viongozi wa vyama vya upinzani ili kuepuka janga hilo kujirudia.
“Serikali iite viongozi wa vyama vya upinzani wayajenge, bila kuwa na mashauriano hakutakuwa na utulivu, hata Uchaguzi wa 2030 hakutakuwa na utulivu kama hakutakuwa na maelewano, maana ukiangalia chanzo cha yote ilianzia malalamiko ya vyama vya upinzani,” amesema Agnes Roman.
Amani Kwibonela, mfanyabiashara katika Soko la Nyankumbu Manispaa ya Geita ambaye duka lake lilivunjwa na bidhaa kuporwa, ameiomba Serikali kwa niaba ya wafanyabiashara walioathiriwa na vurugu hizo, Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia ili kuendelea na shughuli zao.
“Serikali iangalie inatusaidiaje, tulikuwa tunategemea maduka yetu na tuna madeni, lakini kwa sasa hatuna chochote hali ni ngumu. Pia Serikali iwe inafuatilia kwa ukaribu yanayochapishwa kwenye mitandao isiwe inapuuza maana vijana siku hizi wanaamini katika mitandaom” amesema Amani Kwibonela.
Katika zoezi hilo, Tume hiyo pia ilikuwa na wataalamu wa saikolojia ambapo baadhi ya wananchi waliofika kutoa maoni hasa wale waliofiwa na wapendwa wao walipelekwa katika chumba maalumu ili kupewa msaada wa kisaikolojia ili kuwarejesha katika hali ya kawaida.
Pia, Kwibonela ameshauri Serikali kuunda Tume itakayokuwa na jukumu la kufuatilia mwenendo wa uchumi na utekelezaji wa Ilani na ahadi za viongozi wa umma, huku akieleza kuwa chanzo cha vurugu hizo ni kutokana na wananchi kulalamikia baadhi ya ahadi muhimu kutofanyiwa kazi.
Kwa upande mwingine, Msafiri Baruti ambaye ni askari wa Jeshi la Polisi mkoani Geita, ambaye katika vurugu hizo bucha na ukumbi wa kuonyeshea mpira viliharibiwa na waandamanaji, amependekeza uundwaji wa Tume itakayokuwa ikikusanya maoni ya vijana na kuyafikisha kwa Waziri wa Vijana.
“Kila wilaya, mkoa kuwe na Tume inayokusanya mapendekezo ya vijana na kuyatuma kwa Waziri wa Vijana kwasababu kusubiri mpaka afanye ziara inachukua muda mrefu mpaka waziri kufika,” amesema.
Akitolea mfano kwake mwenyewe, amesema alivyohitimu elimu ya sekondari hakuwa na kazi ya kufanya hadi pale alipoamua kwenda Chuo cha Ufundi Veta kusomea ufundi wa magari ambao anabainisha kuwa ulimsaidia.
Baruti amesema kutokana na elimu inayotolewa kutoleta tija kwa vijana katika kujiajiri, ndiyo sababu wengi wao kulalamika ambapo amependekeza maboresho katika sekta ya elimu kufanyika ili kuwapa wananchi ujuzi utakaowawezesha kujiajiri baada ya kuhitimu.
Kiongozi wa Tume hiyo kwa Mkoa wa Geita,Balozi Ombeni Sefue amesema Tume ya kuchunguza matukio ya vurugu za baada ya Uchaguzi, itaendelea kukusanya maoni ya wananchi ili kukabiliana na athari hizo kutojirudia tena.
” Watu wameathirika kwa namna mbalimbali, ni muhimu tusikilize japo kwa uwakilishi lakini tunasikiliza na kupokea maoni pia kutoka kwao juu ya nini kifanyike kwa sababu kote tulikopita wanasema hii siyo Tanzania tuliyoizoea,” amesema Balozi Ombeni Sefue.
