Wawili Yanga watupwa nje, Mudathir arejea kikosini

JANA usiku Yanga ilikuwa uwanjani kucheza mechi ya nusu fainali katika Kombe la Mapinduzi 2026 dhidi ya Singida Black Stars, huku taarifa njema zikiwa ni kurejea kwa kiungo Mudathir Yahya.

Wakati Mudathir akirejea, viungo wawili wa timu hiyo, Aziz Andabwile na Lassine Kouma ilibidi wapewe mapumziko ya muda kutokana na kuumia katika mechi zilizopita za Kombe la Mapinduzi hatua ya makundi.

Wawili hao waliumia katika mechi ya kwanza dhidi ya KVZ, Yanga ikishinda 3-0 ambapo Kouma alitolewa uwanjani mapema dakika ya 14, nafasi yake akachukua Shekhan Ibrahim, huku dakika ya 61, Andabwile naye akatolewa, akaingia  Nizar Abubakar Othman ‘Ninju’.

MUDA 01

Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amesema katika kikosi chake kuna wachezaji wamepata majeraha walipocheza mechi za Mapinduzi, huku wengine wakiwa nayo muda mrefu akiwamo Clement Mzize.

“Ni kweli tumepata majeruhi katika mashindano haya, lakini tunashukuru wengine wanarejea wakiwa wamepona, hii inafanya tuendelee kuwa na kikosi imara cha kupambania mafanikio.

“Tuna kikosi ambacho kina mchanganyiko wa wachezaji, kuna vijana na wazoefu. Tunachofanya kwa vijana kuwapa nafasi kuonyesha uwezo wao na kweli wanafanya hivyo,” amesema Pedro.

MUDA 02

Katika mazoezi ya juzi Alhamisi kabla ya jana Yanga haijacheza dhidi ya Singida, Mudathir alifanya na wenzake mwanzo hadi mwisho akiashiria amepona kabisa.

Kabla ya hapo, tangu Yanga imefika Zanzibar Januari 3, 2026 kwa ajili ya kushiriki Kombe la Mapinduzi, kiungo huyo alikuwa akifanya mazoezi binafsi kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti akiwa sambamba na Mzize kabla ya Jumatano na Alhamisi wiki hii kufanya mazoezi ya timu kwa ujumla.

Mudathir ambaye mara ya mwisho alicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya JS Kabylie iliyomalizika kwa timu hizo kutofungana Novemba 28, 2025, tangu hapo hakuonekana akikosekana mechi mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate na Coastal Union, sambamba na mbili hatua ya makundi Kombe la Mapinduzi dhidi ya KVZ na TRA United.