Wazabuni wazawa wapewa mbinu kushindani zabuni za kimataifa

Mwanza. Serikali imewataka wazabuni, wakandarasi na watoa huduma wa ndani ya nchi kutekeleza kwa viwango vya juu na ubora miradi ya umma wanayopewa ili iwasaidie kuwajenga, kuwatangaza na kuwapa uwezo wa kuchangamkia na kushindania zabuni za kimataifa ili kukuza biashara na maendeleo ya nchi.

Ili kutimiza hilo, wazabuni hao wametakiwa kutumia vyema mafunzo ya kuwajengea uwezo yanayotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) ili kuwaimarisha, kupata soko la uhakika na kuongeza mauzo na mapato.

Vilevile, wameelezwa kuwa kupitia mafunzo hayo wataweza kupata uzoefu na rekodi ya utekelezaji wa mikataba ya Serikali pamoja na uaminifu unaoongeza uwezo wao wa kushindana katika masoko mengine ndani na kimataifa.

Wito huo umetolewa leo Jumamosi, Januari 10, 2026, na Kaimu Katibu Tawala (RAS) wa Mkoa wa Mwanza, Denis Machunda, wakati akizindua mafunzo ya mfumo wa kielektroniki wa manunuzi ya umma (NeST) kwa wazabuni, wakandarasi na watoa huduma za ujenzi zaidi ya 100 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, yaliyofanyika katika ukumbi wa Rock City Mall.

Amesema mafunzo hayo yanawapa uwezo mkubwa wa kushindana ndani na nje ya nchi, huku akiwataka wanapopata zabuni za Serikali wazitekeleze kwa viwango vya juu, kwani kufanya hivyo kutafungua milango ya kupata fursa nyingi zaidi.

“Serikali yetu inatamani sana muongeze ushindani na kushindana kimataifa, mkapiganie hata zabuni mbalimbali nje ya nchi na kuzitekeleza kwa ufanisi. Wajibu wa Serikali ni kuwasaidieni kufikia viwango vya juu kabisa vya ushindani katika zabuni za kimataifa,” amesema Machunda.

Ameongeza kuwa: “Hamna budi kuchangamkia fursa zilizopo katika ununuzi wa umma, kushiriki kwa uaminifu na weledi, na kutumia kikamilifu mfumo wa NeST.

“Kwa kufanya hivyo, mnaweza kukuza biashara zenu, kujenga sifa thabiti katika utekelezaji wa miradi ya Serikali na kunufaika kikamilifu na fursa zinazotolewa na Serikali.”

Machunda amesema Serikali imekuwa ikihimiza taasisi za ununuzi kununua kutoka kwa wazabuni wazawa ili fedha zibaki nchini na kuwanufaisha Watanzania na kuchangia ukuaji wa biashara za ndani na maendeleo ya taifa.

“Nyinyi ni mashuhuda kuwa kabla ya huu mfumo, mchakato wa uombaji zabuni ulikuwa unatawaliwa wakati mwingine na ubinadamu zaidi, lakini lengo la mfumo huu ni kuweka mazingira sawa na kupunguza huo ubinadamu ili kila mtu ahudumiwe kwa viwango sawa, misingi ya ushindani wa haki, usawa na ulinzi wa masilahi ya umma,” amesema Machunda.

Naye Kaimu Meneja wa PPRA Kanda ya Ziwa, Ghatti Chacha amesema washiriki wamefundishwa Sheria ya Ununuzi wa Umma na kanuni zake, pamoja na matumizi ya mfumo wa NeST katika mchakato wa ununuzi unaojumuisha namna ya kujisajili, kuomba zabuni, kuwasilisha malalamiko, na kuwasilisha dhamana za zabuni na utekelezaji wa mikataba.

“Mfumo huu unawasaidia wazabuni wazawa kujua namna ya kuomba zabuni na kupata uzoefu wa kushindana kimataifa,” amesema Ghatti.

Mmoja wa wazabuni walioshiriki mafunzo hayo, Yusuph Nzungu kutoka Ukerewe, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwani yanaongeza ujuzi wa namna ya kuandaa na kuwasilisha zabuni, huku akipongeza PPRA kwa kuondoa upendeleo katika uombaji zabuni.

“Mfumo ni mzuri, umetusaidia hata kama una mtaji mdogo unaweza kupata zabuni kama unakidhi vigezo, na malipo yanakwenda kwa wakati. Nimeanza kuutumia mwaka 2024 na nimepata tenda za kusambaza vifaa katika shule, halmashauri na vituo vya afya,” amesema Nzungu.

Naye Elizabeth Joseph kutoka Tarime amesema mfumo huo una manufaa makubwa kwa wafanyabiashara na kuleta nafuu kwa wazabuni kwa kuwa na uwazi na ushindani sawa bila ukiritimba.