Geita. Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kasala amesisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kushirikiana katika kujiepusha na kuzuia vyanzo vinavyosababisha ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambao hukosa msaada na hatimaye kutapakaa mitaani.
Ametoa wito huo katika hafla ya Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) iliyokuwa inatoa msaada wa Sh50 milioni katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Moyo wa Huruma kilichopo mkoani humo.
“Matatizo mbalimbali katika jamii ikiwemo changamoto zinazotokana na uzazi katika umri mdogo, maambukizi ya virusi vya Ukimwi na ugumu wa maisha yamepeleka uwepo wa watoto wa mitaani wenye uhitaji kutoka katika jamii,” amesema.
“Hivyo, kituo kama hiki, kinatupa somo la kuwapa faraja watoto wenye uhitaji na kuweka jitihada za makusudi za kuzuia ongezeko la watoto hao wanaoishi katika mazingira magumu,” amesema Askofu Kasala.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita (RC), Martine Shigela ameishukuru GGML kwa msaada huo iliyoutoa ambapo inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya uwajibikaji kwa jamii.
Shigela ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, ameipongeza GGML kwa kuendelea kusaidia makundi mbalimbali katika jamii.
“Napenda kuwapongeza GGML kwa ibada hii ya kulea kituo hiki chenye watoto wakiwemo watoto wadogo na wakubwa ambao baadhi yao ni wahitimu wa vyuo vikuu mbalimbali wanaosomea masomo ya sayansi na wale walioajiriwa serikalini ambao wamepitia katika kituo hiki,” amesema.
Hata hivyo, akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mfano wa hundi hiyo kwa uongozi wa kituo hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Duan Campbell, amesema uwepo wa GGML katika moa wa Geita haujikiti tu katika uchimbaji wa dhahabu bali pia katika kuigusa jamii kwa kujenga jamii yenye afya, matumaini na fursa hasa kwa watoto walioko katika mazingira magumu.
“Kujenga jamii yenye afya na yenye matumaini ni sehemu ya jukumu letu kama kampuni inayojishughulisha na uchimbaji wa madini. Uwekezaji wetu katika maendeleo ya kijamii unaendelea kuwa kichocheo cha ukuaji wa ndani, kikanda na kitaifa. Tunajivunia kushirikiana na Moyo wa Huruma na kuona jinsi maisha ya Watoto yanavyobadilika kwa misaada na fursa wanazopata.
“Tunajisikia fahari kuona watoto wanaolelewa katika kituo hiki wanapata mafanikio, ikiwemo wale wanaohitimu katika vyuo vikuu. Hivyo, kama wadau wa maendeleo ya jamii, GGML tutaendelea kuhakikisha kuwa kituo hiki kinapata mafanikio zaidi na kushirikiana na Serikali katika kutokomeza watoto wa mitaani,” amesema Campbell.
Akizungumza baada ya hafla ya kukabidhi hundi, mwakilishi wa GGML kutoka idara mahusiano Mussa Shunashu ameeleza majukumu ya GGML katika kituo hicho kilichoanzishwa kwa ushirikiano kati ya GGML, Jimbo Katoliki la Geita na Halmashauri za Mkoa wa Geita.
“GGML katika kuanzisha na kuendeleza kituo hiki, ilikuwa na wajibu wa kutoa fedha na halmashauri wakati huo ilikuwa na wajibu wa kutoa eneo na Jimbo Katoliki la Geita lilikuwa na wajibu wa kusimamia malezi bora na tunashukuru mpaka leo hii kituo hiki kinaendelea kutoa huduma,” amesema
“Kama ilivyo katika mikoa mingine, mkoa wa Geita pia una watoto yatima, ambao walipoteza wazazi/ walezi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa UKIMWI, hivyo, tuliamua kuwa na kituo hiki kwa msaada wa malezi na elimu kwa watoto wenye uhitaji,” amesema.
Mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho (jina limehifadhiwa) amesema msaada unaotolewa na GGML na wadau wengine umewapa nguvu ya kuota ndoto kubwa.
“Tunajisikia kama tupo nyumbani. Tunathamini sana kuona kuna watu wanaojali maisha yetu na mustakabali wetu,” amesema mtoto huyo.
