BABA AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUMCHOMA MOTO MTOTO WAKE

 ………………..

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Joseph Daudi Mwakalinga maarufu kama Jiggerman, mkazi wa Zimbili, Kinyerezi wilayani Ilala, kwa tuhuma za kumjeruhi mtoto wake kwa kutumia fimbo na moto.

Mtuhumiwa anadaiwa kutekeleza tukio hilo Januari 8, 2026, katika eneo la Kinyerezi, huku jina la mtoto likihifadhiwa kwa sababu za kisheria.

Kwa mujibu wa Polisi, uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo kinyume na sheria, na hatua zaidi zinaendelea kuchukuliwa kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kisheria ili kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ametoa wito kwa wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kuachana na vitendo vya ukatili, hususan dhidi ya watoto, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo.