Bibi wa mke wangu mchawi, nipe mbinu anielewe

Nimeoa mke ambaye wazazi wake walifariki akalelewa na bibi ambaye tunaishi naye kutokana na umri wake na hakuwa na watoto wengine zaidi ya mama yake ambaye amefariki. 

Tulipata watoto watatu wawili wakafariki kiajabu ajabu tu mmoja alitapika mara moja kurudia mara ya pili anapika damu na kufariki papo hapo. 

Taarifa zilizopo kutoka kwa ndugu wa mke wangu huyu bibi yake ni mwanga hata mke wangu amezisikia lakini anazipuuza. Nifanye nini?

Pole kwa kufiwa na watoto wako, naamini machungu yamepoa ingawa si rahisi kusahau Mungu atakutia nguvu na maisha mengine yataendelea.

Kabla ya kupanga mbinu, mikakati ya kumshauri mkeo kuhusu uchawi wa bibi yake na kumuondoa hapo nyumbani  angalia ukweli wa kisayansi na kisaikolojia. 

Vifo vya watoto, hasa wale walio na matatizo ya afya au watoto wachanga, mara nyingi vinaweza kuelezwa kwa sababu za kiafya ambazo zinatofautiana na dhana za kishirikina. 

Tatizo la kupoteza mtoto mara moja au ghafla, kama kutapika damu, linaweza kuwa na sababu za kiasili au za kiafya, maambukizi, au hata tatizo la mishipa ya damu. Ni muhimu kushirikisha madaktari na wataalamu wa afya ili kupata majibu ya kweli badala ya kudhani mambo yasiyo na msingi. 

Ushirikina unapoingizwa kwenye hali hii, unazidisha hofu, huzuni, na migogoro isiyo na sababu halisi, na mara nyingi haileti suluhisho bali unaharibu amani ya familia.

Kumbuka kuwa bibi wa mkeo hana ndugu wala mume mwingine zaidi yenu, kueneza mawazo ya ushirikina ni kinyume na ukweli.

 Najua umeumia kupoteza watoto wawili na unajiuliza inawezekanaje kwa sababu labda wenzako wanaokuzunguka hawajawahi kupatwa na mikasa kama hiyo, lakini si sababu ya kumtuhumu mtu.

 Badala ya kumshinikiza mke wako kuamini mawazo yasiyo na msingi, ni vyema kutumia hoja za ukweli, za kisayansi, na za kihisia: sema unavyohisi huzuni, hofu na mashaka, lakini usiseme kwamba mtu fulani amesababisha vifo kwa njia za kishirikina. Hii itasaidia kuepuka migongano isiyo ya lazima.

Tafuta suluhisho za kihisia na kimaisha. Hali kama hii ni changamoto kubwa, haswa kwa mke wako ambaye anamlea bibi yake aliyemlea wakati hakuwa na wazazi, hivyo kama angekuwa mchawi kama unavyosikia kwa nini asingeanza kumdhuru mkeo? 

Jiulize hili kwanza. Hii inamaanisha kwamba bibi ni sehemu ya historia na hisia zake. 

Najua hali unayopitia kutokana na kufiwa na watoto wako, njia pekee ya kukufanya ukae sawa, kwanza jikite kwenye mazoezi yatakusaidia kuondoa msongo wa mawazo, lakini pia hudhuria vipindi vya mazungumzo na wataalamu wa saikolojia ya familia au mshauri wa ndoa anaweza kukuondoa hofu, huzuni, na mawazo potofu ya ushirikina. 

Hii ni njia ya hekima zaidi kuliko kuruhusu watu wakujaze maneno yasiyo ya msingi ambayo naamini mkeo akiyasikia yatamhuzunisha na akiyaamini itakuwa tabu kwa bibi yake ambaye anamtegemea kwa kila hali.